Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) itafanya mnada wa hadhara wa meno ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa kilo 3,580.29.
Mnada huo utakaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango umepangwa kufanyika Januari 29 kuanzia saa nne asubuhi katika Jengo la Mpingo, Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, zilipokuwa ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (Ivory Room).
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tawa, Dk James Wakibara amesema mnada huo utawahusisha wafanyabiashara wa Nyara waliopewa leseni ya Nyara Daraja la Kwanza mwaka 2017.
Amesema wafanyabiashara hao wataruhusiwa kukagua meno hayo kati ya tarehe 25 na 26 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa na nusu jioni kabla ya siku ya mnada huo.
Amesema wanunuzi watakaoshinda mnada huo watatakiwa kulipa asilimia 25 ya malipo yote papo hapo na asilimia 75 itakayosalia itatakiwa kulipwa ndani ya siku kumi na nne zijazo baada ya mnada huo.
“Mtu yeyote atakayekuwa ametamka bei ya juu, kisha akashindwa kulipa asilimia 25 ya bei aliyotamka, atachukuliwa kuwa ni mwenye kutaka kuvuruga mnada na hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” ameonya mkurugenzi huyo.
Amesema meno hayo yatauzwa kwa wastani wa uzito wa nusu kilo bila kugawanywa au kuchambuliwa wakati wa mnada na wanunuzi wataruhusiwa kuondoa bidhaa kwenye eneo la mnada baada ya kulipia ada na kodi husika kikamilifu na kupewa hati ya kumiliki nyara hizo.