Mgombea Udiwani CCM Atinga Mahakamani Kupinga Matokeo


Mgombea Udiwani CCM Atinga Mahakamani Kupinga Matokeo
Aliyekuwa mgombea udiwani Kata ya Ibighi Wilaya ya Rungwe, Suma Fyandomo kwa tiketi ya CCM ametinga katika Mahakama Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mbeya na kufungua kesi akipinga matokeo yaliyompa ushindi Lusubilo Simba wa Chadema.

Katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika Novemba 26 mwaka jana, Chadema kupitia kwa mgombea wake, Lusubilo Simba ilifanikiwa kutetea kiti hicho kwa kupata kura 1,449 wakati mpinzani wake Suma Fyandomo wa CCM alipata kura 1,205.

Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya msingi, Suma kupitia kwa wakili wake, Daniel Muya leo Jumatano aliwasilisha maombi ya kutaka kupunguziwa dhamana ya gharama za kuendeshea kesi ya uchaguzi mahakamani hapo, lakini upande wa utetezi uliweka pingamizi juu ya maombi hayo.

Mawakili wa upande utetezi ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea Boniface Mwabukusi waliiomba mahakama hiyo kutosikiliza maombi hayo kwa madai kwamba kifungu kilichotumika na mlalamikaji katika maombi hayo kimekosewa hivyo itulipilie mbali shauri hilo.

Hata hivyo, Wakili wa mlalamikaji, Muya alidai mahakamani hapo pamoja na kukosea kifungu kilichotumika lakini hakuifanyi Mahakama kutupilia mbali shauri hilo hivyo aliiomba mahakama kutoa muda wa kurekebisha huku kesi ya msingi ikiendelea.

Baada ya kusikiliza hoja ya pande zote mbili, Hakimu Mfawidhi wa mahakama ya Mbeya, Venance Mlingi aliiahirisha shauri hilo hadi  Januari 15 mwaka huu  atakapotoa uamuzi wa hoja inayobishaniwa.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad