Mke wa Chacha Wangwe Aibuka na Kuiomba Serikali Kufanya Uchunguzi wa Kifo cha Mumewe

Mke wa Chacha Wangwe  Aibuka na Kuiomba Serikali Kufanya Uchunguzi wa Kifo cha Mumewe
Miaka 10 baada ya kifo cha mumewe, mjane wa aliyekuwa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, Ghati, ameiomba Serikali kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha kifo cha mumewe ili haki iweze kutendeka.

Akizungumza mjini hapa juzi kwenye ziara ya mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James, mjane huyo alisema anaamini kifo cha mumewe hakikutokana na ajali ya kawaida bali kilipangwa na baadhi ya watu.

Ghati alitaja majina mawili ya viongozi wa Chadema, akiwatuhumu kuhusika na kupanga njama za kifo hicho kwa sababu za kisiasa.

“Ninayo imani kubwa kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais John Magufuli inaweza kufanya uchunguzi na kubaini kifo cha mume wangu ambacho kilikuwa na utata mkubwa,” alisema.

Mjane huyo mwenye watoto sita, alisema baada ya kijana wake mkubwa Chacha Zakayo aliyekuwa diwani wa Turwa wilayani Tarime kupitia Chadema kujivua wadhifa huo na kuhamia CCM hivi karibuni, kumezuka maneno mengi dhidi ya familia hiyo kukisaliti chama hicho, ilihali kimemhudumia kwa muda mrefu.

Alisema madai hayo siyo sahihi na kwamba tangu mume wake afariki dunia alihangaika na watoto wake peke yake bila msaada wa chama kama inavyodaiwa, huku akiwataka wanaodai kumsaidia kupeleka ushaihidi.

Chacha Wangwe alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Pandambili wilayani Kongwa mkoani Dodoma Julai 28, 2008, alikuwa akitokea Dodoma kuelekea Dar e Salaam ambako alikokuwa akihudhuria vikao vya bunge.

Kufuatia ajali hiyo dereva wake, Deus Malya alishikiliwa na kushtakiwa na hatimaye kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia kwa kuendesha gari kwa mwendokasi na kusababisha kifo na kosa la kuendesha gari bila leseni. Hata hivyo, hukumu hiyo ilitenguliwa baada ya Malya kukata rufaa.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad