Mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani Bi. Beatrice Dominic Kwai, amekanusha taarifa za kuchangia elimu, wafanyakazi wa manispaa hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa www.eatv.tv, Mkurugenzi huyo amesema yeye binafsi hajatoa taarifa yoyote kuomba wananchi wala wafanyakazi wa manispaa hiyo kuchangia elimu, kwani kufanya hivyo ni kukiuka agizo la Rais la kutaka elimu itolewe bure.
"Sina taarifa na hilo, ninachojua mifuko ya elimu ipo kisheria na wa kwangu tunajiandaa kuuzindua, kwakuwa sina document yoyote niliyosaini inayohusiana na michango, na mimi ninatambua maagizo ya Mheshimiwa Rais, siwezi kuchagisha michango ambayo ipo kinyume na utaratibu na sijamuagiza mtu yeyote achangishe", amesema Beatrice Kwai.
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa kuwa wananchi wa Manispaa hiyo pamoja na wanafunzi wametakiwa kuchangia elimu kiasi cha shilingi elfu 5 kila mmoja, jambo ambalo lipo kinyume na agizo la Mheshimiwa Rais Magufuli.