Moto uliozuka ghafla katika makazi ya rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton umezua hali ya tafrani lakini hata hivyo ulidhibitiwa mapema.
Wazima moto karibu na mji wa New York walikimbia nyumbani kwa kiongozi huyo Clinton kukabiliana na moto uliozuka jana Jumatano jioni.
Msemaji wa familia ya Clinton ambaye hakutajwa jina lake alieleza kuwa moto huo ulizuka kwenye nyumba iliyotumiwa na maofisa wa kitengo cha ujasusi cha Secret Service.
Alisema nyumba anayoishi Bill na mkewe Hillary Clinton ambaye wakati fulani alikuwa waziri wa mambo ya nje haikuguswa na moto huo. Nyumba ya Clinton na maofisa usalama zimekaribiana.
Ripoti zinasema kuwa wakati moto huo ukizuka Rais Clinton na mkewe hawakuwepo huku msemaji huyo akifafanua kuwa "kila kitu kiko shwari." Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.
Familia ya Clinton imekuwa ikiishi katika mji wa New Castle, takribani kilomita 64 kaskazini mashariki mwa mji wa New York.