Msimbazi Vigogo Watofautiana Kisa Ujio wa Kocha Mpya

Msimbazi Vigogo Watofautiana Kisa Ujio wa Kocha Mpya
Sakata la kocha mpya wa kurithi mikoba ya Mcameroon, Joseph Omog limegubikwa na utata baada ya vigogo wa klabu hiyo kupishana kauli.

Klabu ya Simba imeanza mchakato wa kusaka kocha mpya baada ya kumtupia virago Omog na nafasi yake kujazwa na Mrundi Masoud Djuma.

Hata hivyo, utata umeibuka kuhusu nafasi ya Omog baada ya vigogo wa klabu hiyo kupigana kumbo kila mmoja akimtaja kocha anayeona anafaa kuinoa Simba.

Habari za ndani zimedokeza kuwa kumeibuka mvutano baina ya vigogo wa klabu hiyo kuhusu kocha sahihi wa kurithi nafasi ya Omog.

“Mvutano ni mkubwa kwasababu kila mmoja ana jina lake mfukoni, lakini ukweli ni kwamba Simba bado haijapata kocha rasmi wa kujaza nafasi ya Omog,”kilisema chanzo hicho.

Wakati Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Mohammed Nassoro akimtaja Mfaransa Hubert Velud kujaza nafasi ya Omog, Kaimu Rais wa Simba, Salim “Try Again” Abdallah amemkana kocha huyo.

Kauli ya Kaimu Rais

Abdallah alisema wanatafuta kocha mpya, lakini sio Velud aliyewahi kuzifundisha timu za TP Mazembe Englebert ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Etoile du Sahel ya Tunisia.

Alisema kumekuwa na taarifa nyingi kuhusiana na kocha huyo, lakini akiwa ndiye kiongozi wa juu wa klabu hatambui ujio wake.

“Habari hizo si za kweli hazina maslahi ya klabu cha kushangaza taarifa zisizo rasmi zimekuwa nyingi, nimeamua kuweka wazi kuhusiana na suala hilo.

“Mimi sijui chochote kuhusiana na suala la kocha huyu anayetajwa sifahamu nani anamleta kwenye klabu yetu, labda kuna klabu nyingine tofauti na Simba. Kwa kifupi hatuna mpango na kocha huyo,” alisema Abdallah.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Nassoro alisema Velud ndiye kocha mpya wa Simba na mchakato wa kumpa mkataba kabla ya kuanza kazi rasmi umeanza.

“Unaulizia mchakato wa kocha, umemalizika tupo katika maandalizi ya mkataba kwa ajili ya kuanza kazi, ”alisema kigogo huyo mwenye ushawishi ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Mmoja wa viongozi wa juu wa Simba ambaye aliomba jina kuhifadhiwa, alisisitiza kuwa Mfaransa huyo ametua nchini na amefichwa kwa ajili ya kukamilisha utaratibu.

Kiongozi huyo alisema Velud aliwasili nchini siku tatu zilizopita kujiunga na Simba, lakini wameshindwa kumtambulisha kwa kuwa hana mkataba.

“Kocha yupo nchini lakini hatuwezi kumtangaza mpaka taratibu za mkataba zikamilike, kuna masuala mengi yanayohusiana na ajira kwa raia wa kigeni ngoja tumalize uongozi utatangaza rasmi,” alisema kiongozi huyo.

Dewji afunguka

Mwananchama mkongwe wa Simba ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kassim Dewji alikataa kuzungumzia suala hilo kwa undani.

“Mimi sijui suala la kocha nilikuwa Kigali, Rwanda nimekuja kuona mechi ya Singida (kesho), kwa kweli sijui lolote wala chanzo chake japo najua klabu kwa sasa haina kocha mkuu,” alisema Dewji na kuomba suala hilo aulizwe Mohamed Nassoro.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad