Mwanachama wa NCCR- Mageuzi, Dk George Kahangwa ametangaza kujiondoa ndani ya chama hicho.
Dk. Kahangwa amesema kuwa haoni dalili yoyote ya mwanga katika chumba cha giza nene linaloighubika NCCR- Mageuzi.
“Mniwie radhi kuwataarifu hili. Sioni dalili yoyote ya mwanga katika chumba cha giza nene linaloigubika NCCR- Mageuzi. Hivyo, hiari ileile niliyoitumia kujiunga, sasa naitumia kukaa pembeni,” ameandia Dk. Kahangwa katika ukurasaw wake wa Facebook.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Dk Kahangwa alipendekezwa na NCCR-Mageuzi kuwania urais ndani ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kupitishwa kupeperusha bendera ya umoja huo.
Hata hivyo, Mkuu wa Oganaizesheni na Utawala wa NCCR-Mageuzi, Florian Mbeo amethibitisha kwa gazeti la Mwananchi kujiondoa kwa Dk Kahangwa.
“Ni kweli amejivua uanachama, alikieleza chama kuhusu suala hilo na hata leo asubuhi nimezungumza naye. Uamuzi aliochukua ni wa kawaida tunauheshimu,” amesema Mbeo.