Dkt. Mwigulu amesema hayo leo wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari baada ya kupata taarifa ya mateso wanayopata baadhi ya wananchi wa Tanzania wanaokwenda kufanya kazi tofauti tofauti nje ya nchi na kusema wameshafanya mawasiliano na Wizara zote zinazohusika na wameshakubaliana kila mmoja kuchukua hatua kulingana na wizara yake.
"Wale watu wanaoweka rehani vijana wetu, wamekuwa wakikimbia hapa na pale na ambao bado hawajakamatwa mpaka sasa waendelee kusakwa wote na wafikishwe katika mkono wa sheria ili sheria iweze kufuata mkondo wake kwa vitendo hivyo vya kinyama na kuwapeleka vijana wetu katika vitendo vya kinyama na kusababisha majonzi kwa familia husika",alisema Dkt. Mwigulu.
Pamoja na hayo na Waziri Nchemba amesema matatizo wanayoyapata vijana hao kwa kisingizio cha kupatiwa kazi nje ya nchi mpaka sasa yamekuwa makubwa mno.
"Tumeona vijana wakiwa wamefungwa miguu vichwa chini na mikono yote huku wakitandikwa viboko kwa madai ya kwamba miongoni mwao kuna aliyewapeleka kuwapa kazi nzuri ya kufanya lakini kwa bahati mbaya wakifika huko wanawekwa rehani kwamba hawataondolewa pale walipo mpaka wale waliowapeleka wakiwa wameshamaliza kupeleka fedha za dawa za kulevya", alisisitiza Waziri Mwigulu Nchemba.