Niyonzima alipatwa na matatizo ya enka na hajacheza mechi yoyote tangu Novemba, mwaka jana, baada ya kuumia mazoezini na kumsababisha kukosa mechi kadhaa za ligi kuu. Yupo nje ya uwanja hadi hivi sasa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Niyonzima alisema kuwa, anajisikia vibaya kuona anakaa nje kwa muda mrefu huku akikosa mechi za ligi, kwa kuwa mpira ndiyo kazi yake anayoitegemea kwa kuwa kukaa nje kutamuathiri.
“Kama binadamu mwingine, siwezi kujisikia vizuri kukaa nje ya kazi yangu kwa muda mrefu, kutaniathiri mimi, maisha yangu ni mpira, kama sichezi mpira, nitajisikia vibaya zaidi ya unavyofikiria kwa kuwa sina kazi nyingine zaidi ya mpira ambao ninautegemea.
“Timu yangu inanihitaji niweze kuisaidia na mimi ninahitaji kuitumikia nisaidie kitu fulani, siwezi kufurahi nipo nje sichezi mpira, furaha pekee niliyo nayo kwa sasa ni kutokana na kuona timu yangu inafanya vizuri kwenye ligi, lakini kuhusu hali yangu sijisikii vizuri kwa kweli.
“Sijajua bado nitarejea lini uwanjani kwa sababu bado naendelea na matibabu, namuomba Mungu anisaidie,” alisema Niyonzima.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, amethibitisha kuwa klabu hiyo itampeleka kiungo huyo nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, baada ya kukamilisha taratibu zote ndani ya wiki hii.
Hata hivyo, Manara amesema nchi watakayompeleka kufanyiwa matibabu wataitangaza baadaye.