Baada ya mchezaji Juma Nyosso wa Kagera Sugar kumpiga shabiki, kamati ya usimamizi na uendeshaji wa ligi imemshitaki kwenye kamati ya Nidhamu ya TFF kwaajili ya hatua zaidi.
Akiongea leo Afisa Mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi Boniface Wambura amesema kamati hiyo imepitia ripoti ya kamishna wa mchezo huo namba 112 kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba SC na kubaini kuwa tukio hilo ni la kinidhamu hivyo kulifikisha sehemu husika.
''Kamati imepitia ripoti ya kamishna na imeonesha kuwa kulikuwa na tukio ambapo mchezaji wa Kagera Sugar Juma Nyosso alimpiga ngumi shabiki hivyo suala hilo limefikishwa kwenye kamati ya nidhamu ya TFF kwaajili ya maamuzi'', amesema Wambura.
Nyosso ambaye bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera anatuhumiwa kwa kumpiga ngumi shabiki baada ya mchezo kumalizika, kitendo ambacho kilipelekea shabiki huyo kuanguka na kuzimia kabla ya kukimbizwa Hospitali.
Katika mchezo huo uliopigwa Jumatatu Januari 22 Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kulipa kisasi cha msimu uliopita ambapo ilipoteza 2-1 kwenye mchezo uliopigwa April 22, 2017.