Picha ya Facebook Yamtia Hatiani kwa Kuua

Picha ya Facebook  Yamtia Hatiani kwa Kuua
Msichana mmoja nchini Canada amepatikana na hatia ya kumuua rafiki yake baada ya polisi kugundua silaha iliyotumika katika tukio hilo kwa kuiona katika picha ambayo wawili hao walipiga na kuiweka kwenye ukurasa wa Facebook.

Cheyenne Rose Antoine, 21, alikiri kumuua rafiki yake Brittney Gargol, 18, mwezi Machi 2015.

Gargol alikutwa amekufa akiwa katika jalala mjini Saskatoon, Saskatchewan, huku mkanda wa Antoine ukiwa karibu na mwili wake.

Antoine alihukumiwa kifungo cha miaka saba kwa kosa la kuua bila ya kukusudia.

Alianza kutuhumiwa kuwa alihusika kuua baada ya kutuma Facebook picha aliyojipiga akiwa na rafiki huyo, ikimuonyesha akiwa amevalia mkanda, saa chache kabla ya Gargol kufariki dunia.

Antoine, ambaye awali alishtakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia, baadaye alikiri kwa kumueleza rafiki yake kuwa alimpiga na kumnyonga Gargol, limeripoti Shirika la Habari la Uingereza (BBC).

Alisema siku hiyo walikuwa wamelewa baada ya kuvuta bangi na baadaye wakazozana vikali.

Polisi walisema taarifa alizowapa awali kuwa walipitia baa tofauti kunywa pombe kabla ya Gargol kuondoka na mwanamume ambaye hakufahamika, wakati akiwa ameenda kumuona mjomba wake, haikujumuishwa kwenye shauri hilo.

Polisi walitumia picha walizotuma kwenye mtandao wa Facebook kubaini mambo waliyofanya siku hiyo.

Polisi walisema taarifa ambazo Antoine alizituma kwenye ukurasa wa Facebook wa Gargol asubuhi ya siku iliyofuata - "Uko wapi? Sijasikia kutoka kwako. Natumaini ulifika nyumbani salama" - zililenga kupotosha ukweli.

Wakati akikiri, Antoine alikubali kuhusika katika kifo cha Gargol, lakini akasema hakumbuki kama alimuua.

"Sitajisamehe. Chochote nitakachosema au kukifanya hakitaweza kumrudisha duniani. Ninasikitika sana... Haikutakiwa iwe hivi," alisema katika taarifa yake iliyotolewa na mwanasheria.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad