Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, linamshikilia Onesmo Machibya maarufu Nabii Tito mwenye miaka 44 ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma, kwa kosa la kueneza chuki ya kidini dhidi ya watu wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Gilles Muroto, amesema Nabii Tito amekamatwa baada ya kurekodi vipande vifupi vya video na picha vyenye maudhui ya kukashifu dini nyingine, na kuleta chuki dhidi ya watu wengine na kurusha mitandao ya kijamii, kinyume na kifungu cha sheria namba 129 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 na marekebisho yake ya 2002.
Aidha, kamanda Muroto amesema mtuhumiwa huyo amesambaza vipeperushi mbalimbali katika maeneo ya starehe akitangaza imani ya kidini inayokiuka maadili ya nchi na kufanya hadharini vitendo visivyofaa, akitumia kitabu kitakatifu cha Biblia.
Nabii huyo amekamatwa akiwa na majoho (kanzu) yakiwa na misalaba miwili, vipeperushi 80, Biblia moja ambayo anatangazia imani inayokwenda kinyume na maadili mema ya taifa.
Nabii Tito kwenye mahubiri yake amekuwa akiwahamasisha watu kutumia vilevi, kufanya maasi, kuoa wanwake zaidi ya mmoja akiwemo msaidizi wa kazi, kitendo ambacho ni kinyume naa maagizo ya kitabu hicho kitakatifu na imani anayoihubiri