Lengo la uongozi wa Rage kuiondoza jezi hiyo kwenye matumizi ya klabu lilikuwa ni kuheshimu na kuthamini mchango wa Mafisango kwa klabu enzi za uhai wake akiwa kama mchezji ambapo mchezaji huyo aliisaidia Simba kubeba ubingwa msimu wa 2011/12, aliiwezesha pia Simba kufika hatua ya 16 bora ya mashindano ya kombe la shirikisho Afrika lakini pia akichangia klabu hiyo kufika fainali ya Kagame Cup ndani ya msimu huo.
Tangu jezi namba 30 ilipotangazwa kustaafishwa , haikuvaliwa na mchezaji yeyote lakini msimu huu imeonekana kutumiwa na golikipa mpya Emanuel Mseja ambaye kwa sasa ndiye golikipa anayekaa benchi Manula akisimama langoni lakini ndiye aliyedaka kwenye michuano ya Mapinduzi Cup 2017/18.
“Lazima nikiri kwamba nimesikitika sana kwa sababu Simba ilikuwa imepoteza mchezaji mzuri na ilimpa heshima, kwa kawaida ni vizuri kuheshimu maamuzi ya viongozi ambao walikuwepo kwenye madaraka. Uongozi mpya unapoingia unaweza ukafanya mabadiko lakini kuna maamuzi mengine huwezi ukayafanya, mimi binafsi jambo hili limenisikitisha sana na nina hakika hawaelewi kama kweli hiyo jezi namba 30 tulikuwa tumesema isitumike tena”-Ismail Aden Rage.
“Kwakuwa wamefanya makosa kwenye mashindano ya kombe la Mapinduzi, nawaomba tumuenzi huyu mchezaji kwa kuhakikisha hii namba 30 haitumiki tena.”
“Bahati mbaya sasa hivi Rais na makamu wake na katibu aliyekuweko hawapo wote sasa inawezekana hawa hawana kumbukumbu na uongozi huu baada ya mimi kuondoka umekuwa unafanya shughuli zake Serena na sehemu nyingine hawana utaratibu wa kufanya shughuli zao kwenye klabu kwa hiyo inakuwa ni vigumu hivyo nikiri pengine kila mtu anastaili yake ya uongozi.”