ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, ameibuka na kusema kuwa, ndani ya klabu hiyo kuna tatizo na kama hawatakuwa makini, basi kuna uwezekano hata ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu timu hiyo ikauokosa.
Rage ameyasema hayo kufuatia Simba, juzi Jumatatu kuondoshwa kwenye Kombe la Mapinduzi, huku pia ikiwa imeshaondolewa kwenye Kombe la FA.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage.
Rage amesema licha ya Simba kuwa vinara wa ligi kwa sasa, lakini kama viongozi, wachezaji na benchi la ufundi hawatakuwa na umoja, timu itavurugana zaidi na kushindwa kufikia malengo.
“Ukiangalia Simba ya msimu huu naona kama imerudia makosa ya Yanga waliyowahi kuyafanya huko nyuma, wamesajili wachezaji wengi bila ya kuangalia uhitaji wa timu zaidi ya kuangalia majina tu. Hili ni tatizo.
“Tatizo lingine ninaloliona ndani ya Simba mpaka kusababisha kufanya kwao vibaya ni kutokuwa na umoja baina ya wachezaji, benchi la ufundi na viongozi, wanatakiwa kukaa chini na kumaliza tofauti zao haraka kabla hatari zaidi haijatokea. Kugombana kumepitwa na wakati.
“Haiwezekani leo hii eti wachezaji wanafanyiwa mabadiliko halafu wanaondoka kwenye benchi, huu ni utovu wa nidhamu.
“Nawasihi wote kwa pamoja wakae chini wamalize tofauti zao wafanye kazi kwani wana kikosi kizuri lakini mambo madogomadogo kama hayo ndiyo yanawasumbua,” alisema Rage.