Rage Hakubaliani na Simba Kumtimua Omog


Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba Alhaji Ismail Aden Rage amesema anaamini kwamba kuna jambo ndani ya klabu hiyo kati ya uongozi, wachezaji na kamati ya ufundi lakini huenda tatizo likawa si kocha na haungi mkono kufukuzwa kwa aliyekuwa kocha mkuu Joseph Omog.

Rage amesema Simba ilifanya makosa kumfukuza omog ambaye aliiongoza klabu hiyo kubeba kombe la FA msimu uliopita lakini pia ameondoka huku timu ikiwa inaongoza ligi huku ikiwa haijapoteza mchezo msimu huu.

”Viongozi wa Simba walifanya makosa makubwa sana kumuondoa Omog, yule kocha alikuwa ameshaweka rekodi nzuri katika klabu Simba, ni muda mrefu sisi hatujashiriki mashindsano ya kimataifa lakini yeye amewezesha tukawa mabingwa wa FA Cup vilevile tumeweza kuongoza ligi hadi sasa.”

“Ukimtoa kocha mkuu halafu kocha msaidizi akapewa majukumu katika mashindano ambayo yana hadhi kubwa haya Mapinduzi nalo hilo nadhani walifanya makosa kama walikuwa na mpango wa kuleta kocha mwingine basi wangetafuta kocha kwa sababu huyu walishamchukua kama msaidizi.”

“Pamoja na matatizo hayo ya kiufundi, ni lazima nikiri kabisa kwamba inaelekea kuna mawasiliano hafifu au kutoelewana baina ya uongozi, wachezaji na kamati ya ufundi. Hapa kuna kitu kinakosekana mimi ningeushauri uongozi wangu wa Simba wajaribu kufanya maongezi kwa sababu nimesoma kwenye mitandao mawazo ya kusema tufukuze au tuadhibu wachezaji ni mawazo yaliyopitwa na wakati. Kinachotakiwa ni kukaa na wachezaji na kuelewa tatizo liko wapi.”

Omog alitimuliwa Simba baada ya kupoteza mchezo wa Azam Sports Federation Cup (FA Cup) dhidi ya Green Warriors ikiwa ni raundi ya pili ya mashindano hayo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad