Sakata la Picha za Utupu Basata Aitawaacha Mastaa Hawa Salama

Sakata la Picha za Utupu Basata Aitawaacha Mastaa Hawa Salama
Muda mfupi baada ya Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Daniel Shonza kumfungia msanii wa filamu na muziki wa Bongo Fleva, Suzan Michael ‘Pretty Kind’ kutojihusisha na masuala ya sanaa ikiwemo kutoweka picha yoyote mtandaoni huku akiwataka wasanii Jane Rimoy ‘Sanchi’ na Gift Stanford ‘Gigy Money’ wafike ofisini kwake, waziri huyo amesema orodha ni ndefu na huo ni mwanzo tu.

Katika mazungumzo maalum na Risasi Mchanganyiko, Naibu Waziri Shonza alisema wizara yake imefikia hatua hiyo baada ya kuona baadhi ya wasanii wakienda kinyume na maadili ya Kitanzania hivyo imelazimika kuingia kazini moja kwa moja kudhibiti mmomonyoko wa maadili.


Akijibu swali la msingi juu ya kwa nini ameamua kuanza na adhabu kali dhidi ya Pretty Kind na siyo wengine, Waziri Shonza alisema: “Unajua kabla ya kutoa adhabu hii sisi kama wizara tulitoa onyo kali kwa watu wanaoharibu maadili yetu kwa kuanika picha za ajabu mitandaoni, lakini yeye aliendelea kwa hatua mbaya zaidi, ndiyo maana tumeona tuanze naye kwa mtindo huo huenda akaelewa serikali inamaanisha nini kuzuia uchafu wa aina hiyo.”

Hata hivyo, Shonza ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum akiwakilisha Mkoa wa Songwe, alisema orodha haijaishia hapo kwani mkononi mwake anayo majina ya wasanii wengi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kuharibu maadili na kwamba muda siyo mrefu wanafuata kwenye kikaango vinginevyo wajirekebishe.


“Orodha ni ndefu na kama mnavyojua wasanii wetu wengi hususan wa kike sijui hudhani kujianika hovyo mitandaoni ndiyo ujuzi wa sanaa au sijui ni nini, sasa wapo wengi ambao muda siyo mrefu nitawafungia kazi kwa adhabu kali zaidi,” alisema Waziri Shonza.

Hata hivyo, Risasi Mchanganyiko ambalo ni namba moja kwa kudodosa habari kwa kina, lilitaka kujua ni adhabu gani watachukuliwa wahusika hao na ni nini kitatokea endapo Gigy Money na Sanchi watakaidi agizo la kufika ofisini kwake ambapo waziri huyo alisema:


“Huwezi kumtangazia adui aina ya silaha ulizonazo, wao kama wanaona tunatania basi waendelee kufanya uchafu wao na hao akina Gigy na mwenzake wasipofika ofisini kwangu kitakachowatokea kitajulikana hapohapo lakini niseme tu kwamba serikali kupitia wizara yangu imeamua kulinda na kupigania maadili ya nchi yetu kwa nguvu zote na hatuko tayari kuaibishwa na watu wachache.”

MASTAA HAWA HAPONI MTU

Licha ya Waziri Shonza kutotaja orodha ya majina ya mastaa wanaosubiri kikaango chao, gazeti hili limedadisi na kubaini kuwa kuna mastaa ambao kama hawatajirekebisha hawatapona. Mastaa hao ni kama vile Agness Mmasy, Amber Ruth, Amber Lulu, Sasha, Tunda, Kidoa na wengine wengi wenye hulka na kariba hizo.

KUTOKA RISASI

Gazeti hili linaipongeza kwa dhati kabisa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kupitia kwa Naibu Waziri Juliana Shonza kwa kuchukua hatua madhubuti kupambana na wasanii wanaotumia kazi yao kuharibu na kumomonyoa maadili yetu badala ya kujenga na kukuza utamaduni wa Kitanzania na tunawataka wasanii kujitambua kama vioo vya jamii.
Chanzo: Global Publishers
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad