Serikali ya Botswana Yamshutumu Trump kwa Kutusi Nchi za Afrika

Serikali ya Botswana Yamshutumu Trump kwa Kutusi Nchi za Afrika
Serikali ya Botswana imemshutumu Rais wa Marekani kwa kusema mataifa ya Afrika ni "machafu" na kusema tamko lake rais huyo ni la kukosa kuwajibika, la kukera na "ubaguzi wa rangi".

Bw Trump alisema hayo alipokuwa akizungumzia sera ya uhamiaji ya Marekani, ambapo alisema anafikiti watu kutoka Haiti, El Salvador na nchi za Afrika hawafai kuruhusiwa kuingia kama wahamiaji Marekani.

Botswana imesema kupitia taarifa kwamba imemwita balozi wa Marekani nchini humo kufafanua iwapo Marekani inachukulia taifa hilo la kusini mwa Afrika kama "taifa chafu" na taifa la mabwege.

Taarifa hiyo ya Botswana imesema tamko la Trump ni la kukosea heshima taifa ambalo lina urafiki wa kufana na uhusiano wa kibalozi.

Botswana imeitaka jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika Sadc pamoja na Umoja wa Afrika kushutumu tamko hilo la Trump.

Bw Trump kwenye Twitter hata hivyo amejitetea na kusema hakutumia maneno hayo, lakini akasema aliyoyasema yalikuwa na "lugha kali".

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema tamko hilo la Trump ni la kushangaza, la aibu na la ubaguzi wa rangi.

Rupert Colville amesema: "Iwapo yatathibitishwa, matamshi haya ni ya kushangaza na ya aibu sana kutoka wka rais wa Marekani, nasikitika kwamba hakuna maneno mengine ya kueleza hili ila kusema kwamba ni ubaguzi wa rangi.

Bw Colville amezungumzia hotuba ya Trump wakati wa kampeni 2016 ambapo alisema wahamiaji kutoka Mexico ni wahalifu na wabakaji.

Na pia, amerejelea tamko lake akijibu maandamano ya waandamanaji watetezi wa ubabe wa Wazungu mwaka jana yaliyokumbwa na vurugu Charlottesville, Virginia walipokabiliana na waandamanaji waliokuwa wanawapinga.

Trump wakati huo alisema "pande zote" zilifaa kulaumiwa.

Afisa huyo wa UN amesema tamko hilo la Trump linaenda "kinyume na maadili ambayo ulimwengu umekuwa ukiazimia kufikia" tangu mwisho wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, na kufungua "mlango wa kuonyesha ukatili zaidi wa binadamu".


Waandamanaji wanaopinga chuki ya rais Donald Trump dhidi ya wahamiaji
Image caption
Waandamanaji wanaopinga chuki ya rais Donald Trump dhidi ya wahamiaji
Alisema: ''Kwa nini tunawaruhusu watu hawa kutoka mataifa 'machafu'"?

Tamko hilo lilidaiwa kuwalenga watu kutoka Afrika, Haiti na El Salvador.

Picha tano za kusisimua mkutano wa Trump na Obama
Trump akataa Air Force One mpya
Ikulu ya Whitehouse haikukana tamko hilo ambalo lilithibitishwa na vyombo vyengine vya habari.

''Wanasiasa fulani wa Washington hupendelea kupigania mataifa ya kigeni, lakini rais Trump atawapigania raia wa M arekani pekee,taarifa iliotoka katika msemaji wa Ikulu Raj Sha ilisema.

Iliendelea: „Kama mataifa mengine ambayo yana wahamiaji wanaofaa kuwa nchini humo, rais Trump anapigania suluhu ya kudumu inazofanya taifa hilo kuwa thabiti kwa kuwakaribisha wale ambao wana mchango katika jamii ,hukuza uchumi wetu na kuingiliana na raia wa taifa letu.

„Kamwe hatakubali mkakati wa muda mfupi ulio hafifu na hatari ambao unahatarisha maisha ya raia wa Marekani, mbali na kutowaruhusu wahamiaji wanaotaka maisha mazuri Marekani ijapokuwa kupitia njia halali."

Matamshi hayo ya rais Trump yanajiri huku wabunge kutika vyama vyote wakimtembelea kupendekeza mpango wa wahamaiji usiopendelea upande wowote.

Seneta wa Democrat Richard Durbin alikuwa akizungumza kuhusu vibali vya muda wa kuishi vinavyotolewa kwa raia wanaotoka katika mataifa yaliokumbwa na majanga, vita ama milipuko ya magonjwa, vilisema vyombi vya habari.

Kulingana gazeti la Washington Post , bwana Trump aliwaambia wabunge kwamba Marekani badala yake inachukua wahamiaji kutoka Norway, ambayo waziri wake mkuu alimtembelea rais Trump siku ya Jumatano.

Seneta Lindsey Graham, ambaye ni mwanachama wa chama cha Republian kutoka Carolina Kusini pia alikuwa katika mkutano huo lakini hakuweza kuzungumzia kuhusu matusi hayo yaliotolewa na rais Trum.

Gazeti la The New York Times liliripoti miaka mitatu iliopita kwamba bwana Trump alisema kuwa raia wa Haiti wote wana ''ukimwi'' wakati wa mkutano wa mwezi Juni kuhusu wahamiaji.

Na kufuatia matamshi hayo rais Trump hakusazwa katika mitandao ya kijamii.

Elijah Cummings, mbunge wa Democrat katika eneo la Maryland alichapisha ujumbe katika mtandao wa twitter akisema: Nayashutumu matamshi hayo yasiosameheka na yanayoshusha hadhi ya afisi ya rais.

Mbunge mwengine mweusi kutoka chama cha Democrat. Cedric Richmond, alisema matamshi ya bwana Trump ni dhihirisho tosha kwamba sera yake ya kuliimarisha taifa la Marekani ni sawa na kulifanya taifa la Marekani kuwa la watu weupe pekee.

Mia Love, raia wa chama cha Republican katika eneo la Utah ambaye pia ni mbunge wa pekee mwenye mizizi ya Haiti nchini Marekani amemtaka rais Trump kuomba msamaha kwa maneno hayo yalio na chuki na yenye kugawanya watu.

Muungano unaopigania haki za watu weusi NAACP ulimshutumu rais Trump kwa kuzidi kuegemea katika ubaguzi wa rangi.

Lakini Ikulu ya Whitehouse imepuuzilia mbalia shutuma hizo zinazomkabili rais.

Afisa mmoja wa Trump alinukuliwa na chombo cha habari cha CNN akisema: Ijapokuwa hili litawakasirisha watu wa Washington, wafanyikazi wanadhani kwamba matamshi hayo yanatokana na mizizi yake, sawa na matamshi yake dhidi ya wachezaji wa NFL waliopiga goti wakati wa kuimbwa kwa wimbo wa taifa.

Msemaji wa ubalozi wa El Salvador mjini Washington alikataa kuzungumzia kuhusu matamshi hayo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad