Serikali ya Tanzania imezifutia usajili meli mbili zilizokamatwa zikiwa na shehena ya madawa ya kulevya na silaha, huku ikikana kuhusika na mzigo uliokatwa nazo.
Taarifa hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu, na kusema kwamba meli hizo zilisajiliwa chini ya mamlaka ya usajili wa usafiri wa baharini, lakini hata hivyo zilishasajiliwa kinyume na sheria.
“Tanzania haihusiki na shehena za silaha wala mdawa ya kulevya yaliyokamatwa ndani ya meli hizo, bali ilitoa usajili wa meli hizo chini ya mamlaka za usajili ambao ni utaratibu wa kawaida wa kimataifa wa kusajili meli duniani, kwa hiyo kufuatia tukio hilo, tumezifutia usajili meli zote mbili, usajili ulitolewa chini ya taasisi ambayo ilishanyimwa kibali cha kusajili meli, na sasa meli zote zimeshusha bendera ya Tanzania ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa”, amesema Mama Samia Suluhu
Sambamba na hilo serikali imesema kuanzia sasa mamlaka husika inapitia taarifa za meli zote zilizosajiliwa nchini ili kuhakiki taarifa zake, na kutoa mapendekezo ya ushauri kwa serikali.
Meli hizo zenye namba za usajili IMO 6828753 ikiwa na kilo 1600 za dawa za kulevya kutoka Jamhuri ya Dominika, na nyingine yenye namba IMO 7614966 iliyokamwa ikiwa na silaha zilizokuwa zikisafirishwa kwenda Libya kinyume na sheria za kimataifa, zilikamatwa Desemba, 2017.
Tunapongeza ufuatiliaji wa serikali juu ya suala hili ila serikali iwaajibishe waliohusika na usajili wa hizi meli kwani inaonekana dhahiri kuwa baadhi ya watumishi wa Serikali wasiowaaminifu wana piga dili katika usajili wa hizi meli za kigeni na wanachokiangalia zaidi ni kujipatia pesa bila ya kujali majanga yanayoweza kuisababishia nchi. Suala la usajili wa meli za kigeni ni sawa na la PASPOTI zetu zinavyotumika vibaya na watu wa mataifa mengine amabao wamezipata kimagendo.
ReplyDelete