Mvutano wa kisheria katika kesi inayowakabili mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga umeibuka kwa mawakili wa pande mbili kuhusiana na ushahidi wa sauti iliyorekodiwa kwa kinasa sauti ambao upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya kuusikiliza na upande wa utetezi kuupinga.
Mvutano huo umeibuka baada ya shahidi wa tano upande wa Jamhuri, Inspekta Joram Magova akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande kudai kwamba ndiye aliyefanya kazi ya kurekodi sauti za Sugu na Masonga kwenye mkutano wao wa Desemba 30 mwaka jana hivyo kuiomba Mahakama kupokea kifaa kilichotumika kurekodia kama kielelezo cha pili kilichowasilishwa na shahidi wa wanne, askari Daniel Masanja katika ushahidi unaondelea kutolewa mahakamani hapo.
Upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu waliupinga ushahidi huo wakiiomba Mahakama kutoupokea wala kusikiliza wakidai shahidi aliyetoa kifaa hicho ana masilahi na kesi hiyo hivyo wanaona ushahidi huo haujakidhi matakwa kisheria.
Hata hivyo, mawakili wa Serikali, Pande na Baraka Mgaya kwa nyakati tofauti, waliinuka na kupinga hoja zilizotolewa na mawakili wa utetezi kwa hoja kwamba walichoiomba mahakama hiyo ni kusikiliza maudhui yaliyomo kwenye kifaa hicho ambacho kimewasilishwa kama kielelezo na kimepokewa.
“Shahidi anapaswa kuwa yule aliyeona, kushuhudia na aliyefanya na kusikia. Sasa hawa wenzetu wanataka kutuaminisha kwamba shahidi siyo yule aliyeona, aliyesikia na kufanya na kushuhudia, kitu ambacho sicho. Kama kielelezo kimepokewa na Mahakama hivyo hoja kwamba kisisikilizwe kilichomo ndani yake, itakuwa imepokea ya nini wakati hatujui kilichomo? Hivyo mheshimiwa hakimu naomba hoja hii itupiliwe mbali.”
Kifaa hicho kilitolewa na shahidi wa wanne Masanja ambaye alidai ndiye aliyekipokea na kukihifadhi katika chumba cha kuhifadhia vielelezo vyote vinavyotakiwa kutolewa ushahidi mahakamani katika Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO).
Shahidi huyo aliongozwa na wakili wa Mgaya na mahojiano yalikuwa:
Wakili: Shahidi hebu tueleze wewe ni nani na unafanya kazi ofisi gani.
Shahidi: Ni askari polisi nafanyia Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO) lakini vilevile ni mtunza vielelezo katika ofisi hiyo.
Wakili: Tangu lini unafanya kazi hiyo?
Shahidi: Tangu mwaka 2004.
Wakili: Vielelezo gani unavyotunza?
Shahidi: Vielelezo vya kesi inayopelelezwa na kuna aina mbili, kwanza vielelezo ambavyo vimeshafunguliwa kesi na pili vielelezo ambavyo kesi yake inakuwa haijafunguliwa mahakamani.
Wakili: Ieleze Mahakama Desemba 30 mwaka jana ulikuwa wapi na ulikuwa unafanya nini?
Shahidi: Siku hiyo majira ya saa 12 jioni nilikuwa nyumbani lakini nikapigiwa simu na Inspekta Joram akinihitaji ofisini niweze kupokea vielelezo.
Wakili: Ulifanyeje baada ya hapo?
Shahidi: Ilinibidi niende na baada ya kufika ofisini nilimkuta Inspekta Joram akanieleza kuna vielelezo vya kuhifadhi, ametoka kwenye mkutano.
Wakili: Mkutano gani?
Shahidi: Mkutano wa Chadema.
Wakili: Ulifanyika wapi?
Shahidi: Ulifanyika maeneo ya Ruanda Nzovwe.
Wakili: Kielelezo gani ulichopokea?
Shahidi: Ni tape recorder.
Wakili: Baada ya kukueleza hivyo ulifanya nini?
Shahidi: Baada ya kuelezwa hivyo, nikavihifadhi kwa kuvifungia kwenye kasiki ofisini.
Wakili: Hebu ieleze Mahakama, Januari 2 mwaka huu ulikuwa wapi na kufanya nini?
Shahidi: Nilikuwa ofisini kwangu nikiendelea na majukumu yangu na akaja Inspekta Joram akihitaji tape recorder ile kwa ajili ya kwenda kuwasikilizishia viongozi wa Chadema akiwamo mbunge (Sugu).
Wakili: Baada ya hapo nini kiliendelea?
Shahidi: Inspekta Joram aliendelea na mahojiano na viongozi hao hadi saa nane mchana akanirudishia kifaa hicho nami nikakihifadhi kwenye kasiki.
Wakili: Tokea siku hiyo ulipokabidhiwa hadi leo (jana) hii nini kiliendelea?
Shahidi: Niliendelea kuhifadhi hadi leo (jana) nilioambiwa vinahitajika mahakamani.
Wakili: Ukiviona unaweza kuvitambua?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Unahitaji Mahakama ifanyie nini vielelezo hivi?
Shahidi: Naomba Mahakama ivipokee kama vielelezo vya ushahidi katika kesi hii.
Wakili: Mheshimiwa Hakimu, shahidi wetu anaomba vidhibiti hivi vyote vipokewe na Mahakama yako kama vielelezo katika kesi hii.
Baada ya wakili kumuongoza shahidi huyo, Wakili Mwabukusi wa utetezi alisimama na kuweka pingamizi juu ya kielelezo hicho akipinga kisipokewe kwa madai kwamba hakijakidhi matakwa ya kisheria na hakina ubora unaotakiwa.
“Kifaa kinachotaka kuwa kielelezo mahakamani hapa ni kifaa ambacho kinasemekana kina maelezo yaliyorekodiwa na mtu mwingine na huyu aliyerekodi hatujaambiwa alirekodi kwa maudhui gani,” Mahakama haijaelezwa kwa namna gani ‘data massage’ zilizomo katika kifaa hiki hazijawa ‘tempered’ na haziwezi kuwa ‘tempered’ kwa namna gani. Tunapinga kifaa hiki kisipokewe kwa vile hakijakidhi matakwa na hakina ubora unaotakiwa kisheria.
Baada ya hoja hizo za Wakili Mwabukusi, Wakili wa Jamhuri, Pande aliinuka na kusema msingi wa hoja hizo unapinga kutolewa kwa kifaa hicho kama ushahidi kwa madai kwamba shahidi aliyewasilisha si aliyerekodi kwamba hawana pingamizi ikiwa kitatolewa na shahidi anayefuata ambaye kimsingi atakitambua.
Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga hoja za wakili huyo na kutaka visipokewe vyote
Mabishano hayo yalidumu kwa takriban nusu saa kabla ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite kuahirisha kesi hiyo kwa nusu saa ndipo atoe uamuzi juu ya kinachobishaniwa.
Baada ya kurejea, Hakimu Mteite alisema Mahakama imejiridhisha kwamba vielelezo hivyo vinaonekana katika muonekano wake halisi, hivyo inavipokea kama vidhibiti na itatoa ufafanuzi wa kwa nini iliamua kuvipokea siku ya hukumu ya kesi yenyewe. Kesi hiyo inaendelea leo.