Tetesi kubwa kwenye soka hapa nchini zinazoendelea kusambaa ni zile zinazohusu klabu ya soka ya Simba kukaribia kufikia makubaliano ya kumwajiri kocha wa zamani wa TP Mazembe Hubert Velud.
Simba ambayo haina kocha mkuu kwa takribani wiki tatu tangu iachane na aliyekuwa kocha wake mkuu Joseph Omog, inadaiwa ipo kwenye maongezi na kocha huyo raia wa Ufaransa mwenye historia kubwa kwenye soka la Afrika.
Velud mwenye umri wa miaka 58, anatambulika vyema kwa mafanikio aliyowahi kuyapata nchini Algeria alipotwaa ubingwa wa ligi nchini humo kwa misimu tofuati akiwa na vilabu vya ES Setif mwaka 2013, 2014 akiwa na USM Alger na Super Cup ya Algeria mwaka 2013 akiwa na USM Alger.
Tayari inadaiwa kocha huyo ambaye msimu wa 2015/16 alikuwa anaiongoza TP Mazembe yupo jijini Dar es salaam na kama maongezi yataenda vyema atatangazwa kuanza kibarua ndani ya vinara hao wa ligi kuu VPL.
Akiwa kocha wa Togo, Velud anakumbukwa kwa tukio la kupigwa risasi kwenye mkono, wakati basi la wachezaji wa timu ya taifa ya Togo liliposhambuliwa na waasi nchini Angola wakati wanakwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010.