Simba vs Singida Utd: Mechi ya Mashambulizi, Wachezaji, Mfumo Kumbeba Hans?

KAIMU kocha mkuu wa Simba, Masoud Djuma ameweka wazi timu yake itacheza mchezo wa kushambulia ili kupata matokeo watakapoikabili Singida United. Mpinzani wake Hans van der Pluijm pia ameitengeneza timu yake katika ‘umbo’ la mashambulizi hivyo mitazamo ya makocha hao wawili kuelekea mchezo wa Alhamisi hii katikas uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni kucheza soka la kushambulia.

Simba wanaongoza msimamo wa ligi wakiwa na alama 26, pointi tatu zaidi ya Singida United walio nafasi ya nne.  Kiufungaji Simba wameonekana kuwa bora zaidi kwa kuwa wamefanikiwa kufunga magoli 25, wakati Singida wamefunga mara 12 tu katika michezo 12. Timu zote zimeonekana kuwa na beki imara kwa sababu zimeruhusu magoli sita-kila timu.

Wachezaji, mfumo, kumbeba Hans

Licha ya kucheza ugenini sitarajii kuona Hans akibadili stahili yake ya uchezaji. Ataendelea kuwapanga walinzi wake wane, Shafiq Matambuze,  Michel Rusheshangoga katika beki za pembeni, Malik Antri na Kenedy Juma katika beki ya kati.

Kwa vyovyote, Djuma atalazimika kuwaanzisha John Bocco na Emmanuel Okwi katika safu ya mashambulizi. kuwapanga Okwi na Bocco kama washambuliaji wawili-pacha kutaifanya Singida kulazimika kumtumia Ken Ally kama kiungo mlinzi zaidi ambaye atakuwa na jukumu la kuwasaidia walinzi wa kati.

Kutumia mfumo wa 3-5-2 kama alivyofanya katika mchezo dhidi ya Ndanda FC, Djuma atakuwa ameruhusu timu yake kuwa hatarini kwa maana Batambuze na Michel ni walinzi wenye uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi timilifu wakitokea pembeni

Hans atawapanga viungo watano katikati ya uwanja. Kenny, Deus Kaseke akishambulia kutokea upande wa kulia, Mudathir Yahya akicheza zaidi na kupanga mashambulizi akitokea kati, Kiggy Makassy akishambulia kutokea upande wa kushoto, Tafadzwa Kotinyu akicheza nyuma kidogo ya mshambulizi Daniel Lyanga.

Ili Simba wafanikiwe kubalansi mechi, wanatakiwa pia kuchezesha viungo wane katika mfumo wa 4-4-2. Erasto Nyoni akicheza katika beki ya kulia atasaidia kuipandisha haraka timu kutokana na mipira yake mirefu inayofika, Asante Kwassi  anaweza kufanya vizuri na kumzima Kaseke kama atachezeshwa beki ya kushoto, Juuko Murshid na Yusuph Mlipili wanafaa kutengeneza beki inayoweza kuifanya timu kujilinda na kushambulia haraka.

Kuwapanga, James Kotei, Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya na Said Ndemla nyuma ya Okwi na Bocco kunaweza kumpa matokeo mazuri Djuma kwa sababu viungo hao wane si wachezaji wanaopoteza hovyo mpira. Simba watatakiwa kuwa makini kwa kuwa Singida wameonyesha nidhamu kubwa ya kimchezo. Wanacheza kitimu, wana nguvu na stamina ya kutosha hivyo hawapotezi hovyo mpira katikati ya uwanja kama wanavyofanya Muzamiru Yassin na Jonas Mkude.

Hii ni mechi ambayo Hans anaweza kushinda kutokana na aina ya mfumo wake na wachezaji alionao na jinsi wanavyojituma. Uzoefu wake dhidi ya Djuma unaweza kumpa matokeo kwa sababu kocha huyo wa Simba ameonyesha kuwa muoga huku akihangaika kujua ni mfumo gani unaifaa timu yake. Nini kitatokea? Ni soka la kasi, ufundi huku mbinu za walimu na uwajibikaji wa wachezaji vikitarajiwa kuamua mshindi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad