Simba Wamemrudisha Mafisango kimyakimya

Mwezi May 2012 klabu ya Simba ilitangaza rasmi kutoitumia tena (kuistaafisha) jezi namba 30 ambayo ilikuwa ikivaliwa na Patrick Mafisango kwa heshima ya mchezaji huyo ndani na nje ya uwanja.

Heshima kama hiyo alipewa kiungo wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Marc-Vivien Foe na klabu yake, Manchester City ya England alipofariki Dunia Juni mwaka 2003, ambapo jezi namba 23 ilitunzwa na kuacha kutumiwa moja kwa moja.

Mwenyekiti wa Simba wakati huo Ismael Aden Rage alitangaza rasmi kuistaafisha jezi ya Mafisango wakati akihutubia mamia ya wadau wa soka waliohudhuria zoezi la kuuaga mwili wa marehemu Mafisango kwenye viwanja vya Sigara Chang’ombe, Dar es Salaam.

“Mafisango alikuwa na mchango mkubwa kwa Simba na mara ya mwisho klabu kukumbumbwa na msiba mzito namna hii ilikuwa ni mwaka 1978 ambapo Simba ilimpoteza mchezaji wake mahiri Hussein Tidwa na ukweli ni kwamba wachezaji hawa tutawaenzi miaka yote na ndio sababu ya kutotumia tena jezi namba 30 kwa kuvaliwa na mchezaji yoyote,” alisema Rage.



Jambo la kushangaza ni kwamba jezi namba 30 ambayo ilitangazwa kustaafishwa kwa heshima ya Mafisango imeanza kutumika tena msimu huu, golikipa Emanuel Mseja aliyesajiliwa kutoka Mbao FC ameonekana akiitumia jezi hiyo.

Inawezekana wadau kibao tayari wameliona hili lakini wameamua kukaa kimya, sio dhambi kwa Simba kuamua kui kuirudisha tena jezi hiyo kuendelea kutumika kwa mara nyingine, lakini ingekuwa jambo zuri kama Simba wangetoka na kuitambulisha rasmi kuitumia jezi hiyo.

Cameroon waliwahi kutangaza kuistaafisha jezi namba 17 ambayo ilikuwa ikivaliwa na kiungo Marc-Vivien Foe ambaye alifia uwanjani wakati akiitumikia timu yake ya taifa kwenye mashindano ya Confederation Cup mwaka 2003 lakini baadae waliirudisha na kuendelea kutumika.

Simba waliamua kumuenzi Mafisango kwa kuistaafisha ya Mafisango kwa lengo la kuenzi na kuheshimu mchango wa nyota huyo lakini yapo mengi ambayo yangefanywa na Simba kwa lengo hilo. Wangeweza kuandaa tuzo ya heshima ambayo wangeipa jina la Mafisango na ingekuwa ikitolewa kwa mchezaji aliyefanya vizuri mwisho wa msimu lakini pia wangeweza kuandaa mashindano ambayo wangeyapa jina la Mafisango.

Mafisango ataendelea kukumbukwa Msimbazi kwa mafanikio ya Simba kwa msimu wa 2011/2012 akiisaidia klabu yake kufika fainali ya Kagame Cup, kutwa bingwa wa ligi kuu Tanzania bara na kufikia hatua ya 16 bora kwenye mashindano wa Kombe la Shirikisho Africa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad