Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, amesema kikosi chao kipo fiti kuivaa Majimaji katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa wa kwanza kwa Kocha Mkuu mpya wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre aliyeanza kukinoa kikosi hicho juzi.
Akizungumzia mchezo huo, Djuma ambaye ni raia wa Burundi, alisema wanauchukulia mchezo huo kwa uzito kwa sababu hawana mashindani mengine makubwa wanayoshiriki zaidi ya ligi kwa michuano ya ndani.
“Mategemeo yetu ni kupata ushindi ili tumalize mzunguko wa kwanza tukiwa tumejiimarisha zaidi kileleni,” alisema.
Kwa sasa Simba inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 32, mbili zaidi ya zile za Azam FC iliyo nafasi ya pili na saba mbele ya Yanga iliyo nafasi ya tatu.
Masoud pia ameuzungumzia ujio wa bosi wake mpya huyo akisema anaamini utaongeza kasi waliyonayo sasa huku akiahidi kumpa ushirikiano wa kutosha.
“Nilikuwa naye siku yake ya kwanza mazoezini (juzi). Kilichotokea ni utambulisho kwa wachezaji wote wa kikosi cha Simba pamoja na kutizama utimamu wa wachezaji,” alisema Masoud.
Miongoni mwa wachezaji waliokuwepo kwenye utambulisho huo uliofanyika Uwanja wa Bandari ni pamoja na majeruhi Haruna Niyonzima, Salim Mbonde na Said Mohammed ‘Nduda’.