Sugu Ahojiwa na Polisi kwa Kutoa Maneno ya Uchochezi


Sugu Ahojiwa na Polisi kwa Kutoa Maneno ya Uchochezi
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda Juu Kusini, Emmanuel Masonga wamehojiwa na Polisi wakidaiwa kutoa maneno yenye lengo la kuleta chuki baina ya wananchi na Serikali katika mkutano uliofanyika Desemba 30, mwaka jana.

Wawili hao walifika Ofisi ya Polisi Mkoa wa Mbeya jana saa nne asubuhi baada ya kuitwa na Mkuu wa Upelelezi wa mkoa huo (RCO) na walitoka saa 9:30 alasiri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga alisema jana kuwa, sababu za kuwahoji Sugu na Masonga ni kupata ukweli wa takwimu za mambo waliyoyazungumza kwa kuwa maneno hayo yanaweza kuleta chuki kati ya Serikali na wananchi.

Kamanda Mpinga alisema, “Katika mkutano ule walizungumza kwamba watu wanauawa na kutupwa baharini mchana kweupe wakiwa kwenye viroba, lakini hawana ushahidi na jambo lenyewe sasa huku ni kuwachonganisha wananchi na Serikali.”

Alisema pia, walitamka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla anamsaidia Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kufanya shughuli zake Mbeya Mjini kwa ajili ya kumuandalia mazingira ya kampeni za ubunge mwaka 2020.

Kamanda Mpinga alisema baada ya kuwahoji waliwaachia kwa dhamana na watakapowahitaji wataitwa na kwamba Ijumaa wanatakiwa kurudi polisi.

Akizungumza baada ya mahojiano hayo, Sugu alisema madai ya polisi ni mwendelezo wa kunyamazisha hoja za upinzani katika kuikosoa Serikali.

Alisema yeye au wapinzani hawatanyamaza kwa namna yoyote ile katika kuikosoa Serikali na viongozi wake na kudai kwamba viongozi wa upinzani kukamatwa imekuwa kawaida hivyo haiwapi shida.

“Nimehojiwa kuhusu maneno wanayodai ni ya uchochezi katika mkutano wangu, nilihoji kuhusu hali ya usalama inayoendelea nchini, watu kupigwa risasi, kuuawa, kutekwa na kupotea katika mazingira tatanishi kwamba hayo yote hayawezi kumletea sifa nzuri Rais,” alisema.

Kwa upande wake Masonga alisema alichozungumza katika mkutano ni kuitaka Serikali kuchukua hatua kuhusu matukio yanayoendelea nchini kwa kuwa yanaleta hofu kwa wananchi.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad