Kocha msaidizi wa Klabu ya Mwadui Jumanne Ntambi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo huko Mkoani Shinyanga, huku chanzo cha kifo chake kikidaiwa ni kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu alilokuwa akisumbuliwa nalo kwa kipindi kirefu.
Hayo yamethibitishwa na Katibu wa Klabu hiyo Ramadhani Kilao wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa 'East Afrika Television' asubuhi ya leo na kusema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa huku akibainisha baadhi ya mambo kuwa ni bado mapema sana kama timu kutoa msimamo wao kuhusiana na kifo hicho cha Ntambi.
"Ni kweli kocha Jumanne Ntambi amefariki dunia kutokana na tatizo la 'presha' lililokuwa likimsumbua takribani wiki moja mpaka umauti ulipomfika. Mpaka sasa bado tunashikilikiana na familia ya marehemu ili tuweze kujua utaratibu mzima ila kitakachokuwa kimejiri tutaikiweka bayana kwa watu wote", alisema Kilao.
Marehemu Jumanne Ntambi alijiunga na timu ya Mwadui FC mwaka jana (2017) wakati michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza akiwa ametokea katika timu ya mkoa wa Moshi.