Uongozi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza jana haukuwa tayari kuzungumzia suala hilo, isipokuwa kampuni ya FastJet ambayo taarifa yake ya jana ilisema ndege yake inaendelea na shughuli zake, huku Mamlaka ya Anga ikilaumu kutokuwepo kwa uzio kuzunguka uwanja huo.
Mtu huyo aligongwa saa 3:00 usiku, kwa mujibu wa FastJet.
Ukweli kwamba mtu huyo alikuwa katika njia ambayo ndege hutumia wakati wa kupaa au kutua bila ya kizuizi chochote, unatia shaka kuhusu usalama wa vyombo hivyo vya usafiri wa anga ambavyo hubeba idadi kubwa ya wasafiri.
Mwandishi wetu wa Mwanza, ambaye hakufanikiwa kupata taarifa zaidi za tukio hilo kutoka kwa wahusika, alisema mazingira ya uwanja huo yanaweka uwezekano wa kuwepo kwa ajali kama hizo.
“Kwa watu wanaoenda au kutoka Kayenze na Igombe, wanaweza kukatisha uwanja wa ndege licha ya barabara kufungwa,” alisema mwandishi huyo wa Mwananchi, Peter Saramba.
“Zamani barabara ilikuwa inakatisha uwanjani, lakini ikafungwa. Kwa sasa barabara ya magari imechepushwa kuelekea ziwani (Victoria), lakini wanaotembea kwa mguu wanaweza kukatisha uwanjani kwa kuwa hakuna uzio.
“Mwenyeji anaweza kukatisha, ila kwa huyo mtu kupita muda huo wa usiku uwanjani, haileti picha halisi ya nini kilitokea na alikuwa anatokea wapi.”
Uwanja wa Mwanza ni moja ya viwanja vikubwa nchini, vikipokea ndege za ndani na nje na unapakana na makazi, kambi ya jeshi na Ziwa Victoria. Kwa sasa Serikali inataka kuupanua.
Katika taarifa yake, FastJet imesema ndege hiyo haikupata madhara na tayari inaendelea na shughuli zake
Msemaji wa FastJet, Lucy Mbogoro alisema ndege hiyo imeruhusiwa kuendelea na safari tangu juzi asubuhi baada ya uchunguzi uliofanywa na mamlaka husika.
“Suala hili tayari limetolewa ufafanuzi na TAA ambao ndio wasimamizi wetu,” alisema.
“Hatuwezi kulizungumzia zaidi ya kuwaomba wateja wetu kutokuwa na wasiwasi kwa sababu ndege yetu haikupata madhara yoyote na inaendelea na safari tangu jana (juzi), baada ya kufanyiwa uchunguzi.”
Kaimu mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Anga (TAA), Richard Mayongela alisema kukosekana kwa uzio kunaweza kuwa chanzo cha mtu huyo kukatiza.
Alisema kabla ya ndege hiyo kuruka, taratibu zote za kiusalama zilifanyika.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vinachunguza tukio hilo kwa kina na tutatoa taarifa kamili uchunguzi utakapokamilika,” alisema.
Hata hivyo, Mayongela anataja uwanja huo kukosa uzio kuwa inaweza kuwa miongoni mwa sababu za mtu huyo kukatisha katikati ya njia ya kuruka na kutua ndege.
“Uwanja wetu wa Mwanza hauna uzio; hii inaweza kuwa chanzo cha mtu huyo kuingia katika njia ya kurukia na kutua ndege,” alisema Mayongela akitoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu
Ili kukabiliana na matukio ya aina hiyo alisema wataimarisha mifumo ya usalama kwenye viwanja vya ndege nchini ikiwemo kuweka uzio kudhibiti watu na vitu visivyotakiwa kuwepo maeneo ya viwanja vya ndege.
Akiwa ziarani mkoani Mwanza Oktoba 30 mwaka jana, Rais John Magufuli aliahidi kuwa Serikali ingetoa zaidi ya Sh9 bilioni kukamilisha ujenzi na upanuzi wa uwanja huo kwa kiwango cha kimataifa kama moja ya mikakati ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa jiji la Mwanza ambalo ni kitovu cha biashara kwa nchi za Ukanda wa maziwa Makuu