Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS) ataondoka saa 2.30 asubuhi ya leo Jumamosi na Ndege ya Shirika la Kenya akiambatana na mke wake, Alicia.
Lissu ametoka hospitalini hapo ikiwa baada ya matibabu aliyoyapata tangu Septemba 7 mwaka jana baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana kwenye makazi yake Dodoma.
Mwanasiasa huyo amesindikizwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na watoto wake pacha, Augustino na Edward, ndugu zake, viongozi na wanachama wa Chadema.
"Nawashukuru sana madaktari wa hapa Nairobi na wale wa Dodoma wakiongozwa na Katibu Mkuu (wa wizara ya afya Profesa Mpoki Ulisubisya waliookoa maisha yangu," amesema Lissu kabla ya kupandishwa gari la wagonjwa
"Nakwenda Ubelgiji kwa matibabu, nikirudi mapambano yanaendelea, nawashukuruni nyote mlioniombea, nawashukuru Wakenya na serikali yao ambao kwa miezi minne nikiwa hapa walinipa ulinzi wakati wote."
Akizungumza kwa msisitizo mbele ya wabunge na wanachama wa Chadema waliokuwapo amesema "Chapeni kazi, mimi nitarudi kuendeleza mapambano haya."
Kuhusu gharama, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema gharama za safari na matibabu zimegharamikiwa na Chadema na TLS.
Wakati baadhi ya waliokuwapo hospitalini kumsindikiza Lissu uwanja wa ndege ni kaka yake Alute Mghwai, mdogo wake, Vinceti Mghwai na ndugu wengine.
Pia, Dk Mashinji, Naibu Makatibu Wakuu, John Mnyika (Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar).
Wengine walikuwapo ni wabuge wa Chadema, Susan Kiwanga (Mlimba) na Godbless Lema(Arusha Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Rose Kamili (Viti Maalum), Anna Gideria (Viti Maalum).
Kwa niaba ya familia, Alute amesema "Tunamwomba Mungu ajalie huko anakokwenda akapate matibabu, kwani alivyokuja hapa sivyo anavyoondoka na tunawashukuru wananchi wa Tanzania na Kenya kwa ushirikiano wao."