Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe ameeleza kuwa hali ya Mbunge Tundu Lissu anayepatiwa matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, imeimarika na hivi karibuni atahamishiwa katika hospitali nyingine kwa ajili ya mazoezi ya viungo.
“Tiba zote ameshamaliza kinachoendelea sasa ni mazoezi,” amesema Freeman Mbowe.
Mbowe amesema hayo leo, Disemba 31, 2017 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa tarehe 6 Januari, 208 Tundu Lissu atasafirishwa kupelekwa katika nchi moja ya Ulaya ambayo hakuitaja kwa kile kilichotajwa kuwa ni kwa sababu za kiusalama.
“Kwa sasa siwezi kuitaja nchi anakokwenda kwa ajili ya usalama,” amesema Mbowe.
Amesema gharama zilizotumika hadi sasa kumuuguza ni dola 300,000 za Marekani sawa na zaidi ya Sh 600 milioni.
Ikiwa ni siku zaidi ya 100, tokea Mbunge Tundu Lissu aliposhambuliwa kwa risasi eneo la nyumbani kwake, Area D, Dododma, majira ya saa 7 mchana, akiwa anatokea kazini, kwa sasa hali yake imeimarika ambapo picha za mwisho kutumwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, zilimuonyesha akiwa amekaa mwenyewe juu ya kitanda cha Hospitali.