Ujenzi wa barabara ya njia sita kuanzia Kimara hadi Kiluvya, unatarajia kuanza mwezi ujao pindi mkandarasi atakapopatikana.
Nyumba takribani 2,000 zilizokuwa zimejengwa ndani ya mita 121.5 ya Barabara ya Morogoro zilibomolewa ili kupisha ujenzi huo ikiwa ni hatua ya awali ya utekelezaji.
Kazi ya ubomoaji iliacha vilio kwa wakazi wa maeneo ya Kimara hadi Kiluvya huku nyumba za kifahari zikiwamo za viongozi wa Serikali na wanasiasa maarufu akiwamo Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kama Profesa J na nyumba ya mke wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa iliyopo Kibanda cha Mkaa Mbezi, zikibomolewa.
Ubomoaji huo pia, ulizikumba nyumba za ibada 32, vituo vya afya vitano, vituo vya mafuta sita majengo ya Serikali manne pamoja na Shule ya Msingi Kimara ambayo ilibomolewa nusu.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake juzi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamkama alisema kazi ya ubomoaji wa nyumba zilizokuwa zimejengwa ndani ya hifadhi hiyo ya barabara imekamilika, hivyo kinachofuata ni maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Tumekamilisha ubomoaji, tunachofanya sasa tupo kwenye hatua ya awali ya kumtafuta mkandarasi ambaye tunatarajia hadi kufikia mwisho wa wiki hii, tuwe tumekamilisha hatua ya awali,” alisema Ndyamkama.
Alifafanua kuwa baada ya hatua hiyo, wanategemea mwezi ujao wawe wamempata mkandarasi na kumkabidhi kazi ya ujenzi.
Ndyamkama pia alisema kwa upande wa majengo ya Serikali likiwamo jengo la Tanesco, bado wanaendelea na ubomoaji lakini kuna baadhi ya nyumba chache za wananchi maeneo ya Kibo wanaendelea kubomoa wenyewe.
“Kwa sasa hatumshinikizi mtu kubomoa, wanabomoa wenyewe, maana asilimia kubwa ya ubomoaji imekamilika tunachofanya ni maandalizi tu ya kuanza ujenzi rasmi,” alisema.
Alifafanua kuwa ujenzi huo ukikamilika utasaidia kupunguza msongamano katika barabara ya Morogoro ambayo imekuwa kero ya muda mrefu.