Rwebangira alidai kwamba kuonekana kwa gari hilo ni njama za Chadema kutaka kuvuruga uchaguzi wa Februari 17 na kwamba tayari wamefikisha suala hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni ambako dereva wake anashikiliwa pamoja na gari hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo alithibitisha kukamatwa kwa gari hilo na kusema, “Gari lilikuwa linachunguzwa tangu jana, sasa muda mrefu umepita, sijui wamefikia wapi katika uchunguzi huo.”
Hata hivyo, uongozi wa Chadema umekanusha kula njama dhidi ya CCM na kusema kwamba hiyo ni mbinu za chama hicho tawala kutaka kuvuruga uchaguzi.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita hakupatikana mara moja kuzungumzia tukio hilo lakini Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi alisema kwamba jana usiku baada ya kikao cha tathmini Mwita alilalamika kwamba dereva wake haonekani.
Ole Sosopi alidai kwamba CCM wanataka kutengeneza mazingira ya kuvuruga uchaguzi huo kwa kisingizio kwamba Chadema ndiyo wameanzisha.
“Inawezekanaje dereva wa Chadema akaenda CCM! Kufanya nini? Wanajaribu ku pre-empty ili zikitokea fujo waseme ni sisi. Ninaomba jeshi la polisi wachukue hatua, kwa sababu hali hii haikubaliki,” alisema Sosopi.
Alidai kwamba dereva huyo alitekwa na watu wa CCM kuanzia saa tisa alasiri na akaachiwa saa kumi na moja alfajiri baada ya kumtesa.
Akizungumzia tukio hilo jana, mwenyekiti huyo wa UVCCM, alisema dereva huyo wa meya alikamatwa jana saa 2:30 usiku katika ofisi za CCM Kinondoni na alipoulizwa alitoa sababu tofautitofauti kwamba alikwenda kuegesha na sababu nyingine kuwa alimpeleka meya Mwita kwenye mkutano maeneo ya jirani.
“Tulipekua simu ya dereva na kubaini mawasiliano kati yake na meya wa jiji akimuuliza “Uko na nani hapo?”, “Mpango unakwendaje?”. Zote hizo ni njama za wenzetu kutaka kuvuruga uchaguzi, sasa tunaliomba jeshi la polisi lifanye kazi yake kwa haki,” alisema Rwebangira.
Alidai kwamba vijana wawili waliokuwa kwenye gari hilo walitoroka lakini walitambuliwa kwa jina moja moja la Godfrey na Alex na kwamba watalisaidia jeshi la polisi kuwapata kwa sababu wanafahamika kwa vurugu huko Kigamboni.
“Tumekuwa tukipokea taarifa kwamba ofisi ya meya inatumika vibaya. Hatuwezi kuacha mambo haya yakaendelea, lazima vyombo vyetu vya dola vichukue hatua,” alisema mwenyekiti huyo.