Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA) Mchungaji Peter Msigwa amesema kuwa viongozi wa CHADEMA na baadhi wanachama wa CHADEMA Iringa Mjini wamekamatwa na polisi wakihusishwa na uchomaji wa nyumba ya kiongozi wa CCM na ubomolewaji wa nyumba.
Msigwa amelaani kitendo cha jeshi la polisi kuwakamata baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA kwa kuhusishwa na vitendo vya kuuungua kwa nyumba na kubomolewa nyumba na kudai kuwa jeshi hilo kwa sasa lilipaswa kuanza Intelijinsia ili kujua kwanini nyumba hiyo imewaka moto na nyingine kubomolewa kuliko kufanya uchunguzi jambo ambalo linaweza kupelekea kuwatia hatiani watu wasiohusika.
"Polisi Iringa acheni mara moja kamata kamata ya Vijana Iringa Mjini kwa tuhuma za kuchomwa nyumba Moto na kubomolewa nyumba. CHADEMA haina visasi vya damu katika 'struggle' ya Demokrasia Nchini. Kuhusisha uharibifu wa aina hii na siasa ni kukosa weledi na maarifa katika uchunguzi" alisema Msigwa
Aidha Mchungaji Msigwa amesema kuwa kuhusu nyumba kuungua moto huwa kuna vyanzo vingi vinavyosababisha jambo ambalo polisi walipaswa kwanza kutulia na kuvipa nafasi vyombo husika kuweza kujua chanzo cha moto huo, badala ya kuanza kulifanya tukio la kisiasa.