SHIRIKA la Posta Tanzania, limeokoa viwanja vyake 198 katika maeneo mbalimbali nchini, vilivyokuwa vimeingia kwenye mikono ya wajanja wachache kwa ajili ya kujimilikisha.
Aidha, shirika hilo limedhibiti matumizi mabaya ya fedha, kujimilikisha mali za shirika na ubadhilifu mwingine uliosababisha kujiendesha kwa hasara na mali zake kupotea ovyo kwa miaka tisa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta, Dk. Haroun Kondo, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, walipoingia mwaka jana walikuta vinavyoendelea ni wizi, rushwa na ubadhilifu, huku mali nyingi za shirika zikiwa hazijaorodheshwa kokote.
“Tuliamua kufanya ziara mikoani. Wapo waliolalamika kwamba tunasafiri sana, lakini hilo lilitusaidia kujua mali za shirika zimemilikishwa watu. Tulienda mahali tukakuta kuna kituo cha mafuta imejengwa kwenye kiwanja cha Posta na hawajui kwamba ni mali yao, hawajawahi kukusanya hata senti moja,” alisema.
Alisema waliingia kukiwa hakuna fedha benki na Sh. bilioni 4 zimetumika nje ya matumizi, madeni zaidi ya Sh. bilioni 16 hayajakusanywa na walipokusanya (Bodi) Sh. bilioni 10 zikaishia mifukoni mwa wajanja.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Posta ilikuwa na akaunti za benki zipatazo 120, jambo lililozua shaka na bodi iliamua kuzifunga.
Alisema pia walipitia upya mikataba na watoa huduma mbalimbali, ubia katika maeneo ya matengenezo ya magari na usafirishaji wa vifurushi na kubaini ubadhilifu mkubwa, hivyo kuamua kufuta baadhi ya mikataba na mingine inaendelea kupitiwa.
“Kutokana na hayo wapo watumishi walifukuzwa, walifikishwa mahakamani, walikabidhiwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuwanyang’anya mali za shirika walizojimilikisha pamoja na kuondoa wafanyakazi 95 kwa kosa la vyeti feki,” alisema.
Dk. Kondo ambaye pia ni Luteni Kanali mstaafu wa jeshi, alisema wamekuja na mkakati mpya wa kuijenga Posta mpya kwa kununua magari madogo sita, malori matano na mabasi matatu.
“Shirika lilishindwa kutoa huduma vizuri kutokana na uchakavu wa magari. Tumeingia makubaliano na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kusambaza dawa mikoani kwa kutumia magari yetu 10. Tunaomba serikali iendelee kutumia huduma zetu ili tupate kipato zaidi,” alibainisha.
Aidha, alisema wanajiendesha bila ruzuku ya serikali na kuiomba kuiona ni Posta mpya na iwapo serikali itatumia huduma zake kama kusafirisha vifurushi, itawawezesha kupata mapato na kuchangia pato la Taifa. Posta ‘Express’
Alisema Shirika hilo limeanzisha huduma Posta haraka kwa huduma zote kupatikana eneo moja na kuiomba serikali kuruhusu huduma za pasi za kusafiria na leseni kutolewa kwenye eneo la Posta.
Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Hassani Mwang’ombe, alisema uwapo wa kituo cha posta ‘Express’ kutawezesha wananchi kupata huduma sehemu moja na iwapo huduma za leseni na pasi za kusafiria zitaongeza mapato ya posta.