Vumbi Lazidi Kutimka Uchaguzi Mdogo Siha

Vumbi Lazidi Kutimka Uchaguzi Mdogo Siha
Chama cha Wananchi CUF, kimezindua kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Siha kikiwataka wananchi kumchagua mgombea wake Tumsifuel Mwanri kwa kuwa ana uwezo wa kuwaletea maendeleo ya kweli.

Wakati CUF ikisema hayo, mgombea wa chama cha Sau ameahidi kutoa nusu ya mshahara wake kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hizo uliofanyika Miti Mirefu, naibu mkurugenzi wa ulinzi na usalama CUF, Masoud Omar alisema vyama vingine vilipewa dhamana ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Siha lakini vimeshindwa hivyo wamchague Mwanri kwa maendeleo yao.

“Tunawashangaa kwa kushindwa kuleta maendeleo na kuanza kugombana wao kwa wao, sasa CUF tumewaletea jembe la kuwaletea maendeleo, mchagueni alete mabadiliko Siha,” alisema.

Akiomba kura, Mwanri alisema endapo atapata ridhaa ya kuongoza, ataboresha maendeleo katika sekta ya elimu, kilimo na maji.

Alisema atawatafutia wananchi masoko ya bidhaa za kilimo na kwa wafugaji, soko la ngozi ili waweze kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi. Pia aliahidi kutafuta mashamba kwa ajili ya kilimo kwa shule, lengo likiwa ni kuwapunguzia wazazi mzigo wa michango ya chakula.

Wakati mgombea huyo wa CUF akitoa ahadi hizo, mwenzake wa CCM, Dk Godwin Mollel amesema akiwa upinzani, alizuiwa na kuonywa mara kwa mara pale alipojaribu kuunga mkono mazuri yaliyofanywa na Serikali.

Alisema kauli ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa walioko upinzani wanaweza kumuunga mkono Rais wakiwa huko bila kuhama ni ya matumaini kwa viongozi wa chama hicho wakiwamo wabunge ambao wamekuwa na kiu ya kuzungumzia mazuri yanayofanywa na Serikali na kuhofiwa kuonywa na kuhojiwa.

Akijibu kauli ya Mbowe aliyoitoa hivi karibuni, Dk Mollel aliwaambia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana eneo la Zahanati ya Ormelili kwamba wamchague hata kama yeye ni gunia la misumari. Akimnadi mgombea ubunge wa Chadema katika Viwanja vya Ngarenairobi, Mbowe, alinukuliwa akisema kuwa Dk Mollel ni gunia la misumari.

Dk Mollel ambaye hivi karibuni alijivua ubunge wa Siha baada ya kujiondoa Chadema na kuteuliwa na CCM kugombea tena nafasi, alisema kama yeye ni gunia la misumari ni vizuri akapewa nafasi hiyo kwani atatumiwa kukamilisha miradi.

Akimnadi mgombea huyo, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, aliwaahidi wananchi wa Siha kuletewa maendeleo na Kata ya Endument kupewa ekari 4,000 kwa ajili ya makazi, endapo wataichagua CCM.

Katika kampeni zake, mgombea wa Sauti ya Umma (Sau), Mdoe Azaria alisema kuwa endapo atapata ridhaa ya wananchi, atatoa nusu ya mshahara wake katika halmashauri kwa ajili kutekeleza miradi.

Alisema fedha hizo zitakuwa zinasaidia wananchi wanaoshindwa kutoa michango inayohitaji na kutumika kwenye huduma za afya kwa ajili ya watu wasiokuwa na uwezo.

Alisema Siha imekuwa na migogoro mingi ya ardhi kutokana na baadhi viongozi kuwa mikononi mwa watu binafsi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad