Wafanyabiashara Waijia Juu Serikali

Wafanyabiashara Waijia Juu Serikali
Wafanyabiashara nchini wameiomba Serikali kuacha kufanyakazi kwa kukurupuka ikiwamo kuwaadhibu kwa makosa ya wengine badala yake iwe kitu kimoja na sekta binafsi ambayo ina mchango mkubwa kwa Taifa.

Wito huo ulitolewa jana na makamu mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte kwenye mkutano baina yao na Serikali ulifanyika katika ukumbi wa Hazina mjini hapa na kuhudhuriwa na wabunge na baadhi ya mawaziri.

Shamte alisema katika baadhi ya maeneo, Serikali imekuwa ikifanya mambo kwa kukurupuka na kujikuta ikiwaumiza wafanyabiashara ikiwamo masuala ya kodi.

Makamu mwenyekiti huyo alisema sekta binafsi inaumizwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wa kukurupuka hasa wa kuwaadhibu watu wasiohusika kwa kosa la mtu mmoja.

“Wakati mwingine watu wanaumizwa sana kwa ajili ya maamuzi haya, kodi na kufunga biashara za watu ilhali kosa linakuwa la mtu mmoja. Kwa nini hamuondoi kasoro hiyo?” alihoji Shamte wazo ambalo liliungwa mkono na mkurugenzi mtendaji wake, Godfrey Simbeye.

Akijibu hoja hiyo, waziri wa fedha na mipango, Dk Philip Mpango alikiri kuwapo kwa uamuzi wa kushtukiza serikalini na kusema wakati mwingine inalazimika kufanya hivyo.

Dk Mpango alisema wakati mwingine kuna madhara kwa watu kukurupuka na kufanya vitu visivyokuwepo na kusema ndani ya Serikali, kuna baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu ambao wanafanya vitu ama kwa kukurupuka au kutokujua.

“Nakiri kweli ndani ya Serikali kuna watu ambao wanafanya mambo ya ovyo na kuisababishia Serikali hasara kubwa, lakini kuna wakati tunafanya hivyo kwa sababu inabidi tufanye hivyo kwa masilahi ya nchi,” alisema Dk Mpango.

Hata hivyo, aliwatupia lawama baadhi ya wafanyabiashara akisema wamekuwa na tabia ya kukwepa kodi jambo ambalo ni kinyume na Serikali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad