Wagonjwa 40 jana Jumatano Januari 10, 2018 wametumia usafiri wa basi kuhamishwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwenda Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila, iliyopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Safari ya wagonjwa hao ilianza saa 9 alasiri baada ya kutolewa katika wodi zao kwa msaada wa wauguzi na madaktari kwa kutumia baiskeli za wagonjwa, kupandishwa katika basi hilo aina ya Coaster.
Mwananchi ilishuhudia baadhi yao wakishindwa kutumia baiskeli hizo, kulazimika kutolewa wodini wakiwa katika vitanda.
Walipoingizwa katika magari hayo, baadhi walishindwa kuketi, kuamua kulala katika viti vya vyuma vya basi.
Hata hivyo, utaratibu huo wa kuwahamisha, MNH ilihakikisha kila mgonjwa anakuwa na ndugu mmoja ambaye aliambatana naye katika safari hiyo.
Mmoja wa ndugu wa wagonjwa hao, Jenifer Kimaro amelalamikia utaratibu huo kwa madai kuwa wagonjwa hawawezi kuwa salama kutokana na umbali kutoka Muhimbili hadi Mloganzila.
"Nafikiri wangetumia gari la wagonjwa ingekuwa salama zaidi, huu usafiri waliotumia si sawa,” amesema.
Alipoulizwa sababu za kutumia basi badala ya magari ya wagonjwa, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma MNH, Aminiel Eligaesha amesema wamelazimika kufanya hivyo kutokana na wingi wa wagonjwa.
"Wagonjwa ni wengi wanaotakiwa kuhama na hatuwezi kutumia magari ya wagonjwa kwa wote 40 na leo pia tunatarajia kuhamisha wengine 40. Tunaowahamisha si wagonjwa mahututi,” amesema.
Kuhusu kutotumika kwa magari ya wagonjwa amesema magari hayo yana uwezo wa kubeba mgonjwa mmoja tu tofauti na basi linaloweza kubeba idadi kubwa zaidi.
"Tulizungumza nao kwamba wale wagonjwa wenye uwezo wa kukaa wapande kwenye basi na wasioweza kukaa tunawahamisha kwa kutumia magari maalum ya kubebea wagonjwa. Mabasi yanayobeba wagonjwa huongozwa na gari mbili za kubebea wagonjwa ili kutotumia muda mrefu njiani,” amesema.
Jana Serikali ilihamisha rasmi idara ya magonjwa ya ndani kutoka MNH kwenda Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kampasi ya Mloganzila (MAMC).
Uteketezaji huo umekuja mwezi mmoja baada ya Rais John Magufuli kuzindua hospitali hiyo na kutoa maagizo kuwa baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika jengo la Mwaisela wahamishiwe MAMC ili kupunguza msongamano uliopo katika jengo hilo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema wagonjwa watakaohama ni pamoja na wale waliopo katika wodi namba 3,4,5,6,7 na 8 zilizopo kwenye jengo la Mwaisela, na haitahusisha wale walio mahututi na wenye sababu maalum.