Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) Injinia Elius A. Mwakalinga ametolea ufafanuzi taarifa za serikali kuvunja mkataba na wao, baada ya kutoa taarifa za uongo kwa Waziri Mkuu.
Akizungumza na mwandishi wa www.eatv.tv Injinia Mwakalinga amesema yeye kama Mkurugenzi taarifa hizo hazijamfikia rasmi, na iwapo zitamfikia ana uhakika atakuwa na taarifa za kutosha na kuwaeleza wananchi nini kilichojiri.
“Mimi taarifa hizo ndio nazipata kwako, sijapokea taarifa yoyote kuhusu suala hilo, na unapovunja mkataba kuna watu wawili waliosaini huo mkataba, na mimi ni client, hivyo kama nitapewa taarifa rasmi kwa barua basi lazima umma utajulishwa, kwani ndio utaratibu wa kazi”, amesema Injinia huyo.
Pamoja na hayo Injinia Mwakalinga amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia masuala yote ya TBA kwa kuwa ndani yake kuna watu wengi, hivyo watatoa taarifa rasmi juu ya masuala yote ambayo wamekuwa wakilaumiwa na kunyoshewa kidole.