Walimu ‘Watemwa’ kwa Utoro, Wanafunzi Washindwa Kumaliza kwa Mimba

Walimu ‘Watemwa’ kwa Utoro, Wanafunzi Washindwa Kumaliza kwa Mimba
Walimu tisa wa shule za msingi wilayani Bahi wamefukuzwa kazi kutokana na utoro huku wanafunzi sita wakishindwa kumaliza elimu ya msingi kutokana na mimba.

Ofisa elimu na taaluma wilayani humo, Issa Nchila ametoa taarifa hiyo leo Jumatano kwenye kikao cha wadau wa elimu waliokutana kujadili changamoto zinazosababisha wilaya hiyo kuendelea kushuka kielimu.

Nchila amesema walimu hao walikuwa miongoni mwa walimu 11 waliokuwa wameshtakiwa kwa makosa mbalimbali ya utoro na nidhamu kazini.

Amesema walimu wawili kati ya hao, walishushwa vyeo ikiwemo kupunguziwa mishahara yao.

Ofisa huyo amekiri hali mbaya kwa matokeo ya elimu huku wilaya ikiwa imeshika nafasi ya tano katika halmashauri 8 za Mkoa wa Dodoma.

"Bado tutaendelea kuwachukulia hatua kali kwa kushirikiana na TSD ili kukomesha vitendo hivyo kwani ni moja ya mambo yanayotukwamisha na kufanya watoto wetu wafanye vibaya," amesema Nchila.

Amesema bado wilaya inakabiliwa na mdondoko mkubwa wa elimu kwani wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza walikuwa  4,564 lakini waliofanya mtihani wa darasa la saba ni wanafunzi 3,005 huku watoto 1559 wakiishia njiani.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu amesema wilaya hiyo ina tatizo la mimba kwa shule za msingi na sekondari ambalo watalikomesha.

Kitundu amewaambia wadau wa elimu kuwa mimba zinamkera wakati wote anaposikia watoto wanashindwa kumaliza elimu zao huku wadau wakishindwa kutoa ushirikiano wa kuwabaini wahusika.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad