Jumla ya wanafunzi watano wa kike wa shule za sekondari Tandahimba waliopata mimba mwaka 2017 wamekamatwa pamoja na wazazi watano baada ya kufanyika msako na kufanikiwa kukamatwa kwa watu hao.
Katibu Tawala wa wilaya ya Tandahimba, Mohamed Azizi amesema hayo jana Jumamosi kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo, Sebastian Waryuba baada ya kufanikiwa kuwakamata wanafunzi hao wakiwa na watoto wao huku wahusika ambao wamewasababishia kukatiza masomo yao kutokomea kusikojulikana.
“Tumefanikiwa kuwakamata wazazi na wanafunzi watano wakiwa wamejifungua kati yao mmoja ameacha shule akiwa kidato cha nne, huku mwingine tatu na kidato cha pili baada ya kuzungumza nao wote wamesema hakuna hata mmoja ambaye anapata huduma kutoka kwa wahusika ambao wamewapa mimba hali ambayo inawapa shida wazazi wao kuwahudumia,” alisema Azizi
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mkolea, Selemani Abduli amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa mkuu wa shule hatua ambazo amezichukua ni kuwakamata wahusika wote wawili na kuwapeleka katika kituo cha polisi kilichopo wilayani humo.
“Hatua ambayo nilichukua baada ya kupata taarifa kwa wakuu wa shule ni kuwatafuta wanafunzi ambao wamepata ujauzito pamoja na wahusika kuwapeleka kituo cha polisi lakini wahusika wakifika kituo cha polisi waliachiwa,” alisema Abdul
Akizungumzia tukio hilo mmoja wa mzazi ambaye mwanaye amekatiza masomo yake kutokana na kupata ujuzito Hassan Mfaume amesema amesikitishwa baada ya kusikia mwanaye amepata ujauzito hali ambayo imepelekea kukatiza masomo yake.