Mrembo wa sinema za Kibongo, Wema Sepetu amejikuta akiingia matatani kwa kudaiwa ‘kuwafuga’ wanaume wanaodaiwa ‘si riziki’ (mashoga) nyumbani kwake, Salasala.
Kwa mujibu wa chanzo makini, mrembo huyo amekuwa akiishi na wanaume hao tata kwa muda mrefu jambo ambalo limekuwa likiwakera majirani wanaomzunguka na kuwafanya wamshitaki serikalini.
“Unajua hii tabia yake si ya leo, ameanza muda mrefu na amekuwa akiwakera majirani zake kwani wanahofia kuharibiwa watoto wao wa kiume kwa kufuata matendo yao,” kilidai chanzo.
Kikizidi kushusha madai hayo chanzo hicho kilienda mbali zaidi kwa kusema mrembo huyo ni sikio la kufa kwani alikuwa akiishi na mashoga hao tangu alipokuwa anaishi maeneo ya Ununio jijini Dar hadi kumsababishia matatizo pia. “Kule Ununio alikuwa nao hawa mashoga, sijui ni marafiki zake au ni watu wa aina gani kwake.
Watu wengi wanajiuliza kwanini anawakumbatia, wanakosa majibu. “Kama mnakumbuka vizuri hata mama yake aliwahi kwenda kuwatimua mashoga hao baada ya kuona wanamharibia lakini sijui Wema anawapendea nini, bado yuko nao tu,” kilizidi kumwaga ubuyu chanzo hicho. Baada ya kunasa ubuyu huo, wanahabari wetu walifika nyumbani kwa Wema alikohamia kwa sasa, Salasala jijini Dar ili kuweza kujionea mashoga hao lakini ilishindikana baada ya kugonga geti muda mrefu bila kufunguliwa.
Hata hivyo, Ijumaa lilifanikiwa kuzungumza na mjumbe wake wa nyumba kumi, Marko Mbaku ambaye alisema taarifa za uwepo wa mashoga amezisikia lakini ameshindwa kupata ushirikiano kutoka kwa Wema.
“Kwanza niseme tu simtambui Wema maana hajaja hata kujitambulisha kwangu tangu amehamia hapa, nimeletewa malalimiko mengi dhidi yake lakini kila nikimpelekea barua hajibu chochote wala haji,” alisema mjumbe huyo na kushauri waandishi waende ofisi za serikali ya mtaa kwani kuna taarifa zaidi.
Ijumaa lilifika Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Salasala na kuzungumza na wajumbe wake ambao kwa pamoja walikiri kuwepo kwa mashoga nyumbani kwa Wema na kushauri waandishi wazungumze na mwenyekiti wao kwa taarifa zaidi.
Alipotafutwa Mwenyekiti Hashim Bakari, alikiri uwepo wa malalamiko hayo ofisini kwake na kwamba wanajipanga kwenda kuzungumza na mrembo huyo ili kama atashindwa kuwatoa, basi wamhamishe mtaa.
“Ni kweli malalamiko hayo yapo, tunajipanga kwenda kumuona Wema Sepetu ili kama wapo hao mashoga awaondoe, akikaidi tutamhamisha hapa mtaani kwetu,” alisema mwenyekiti huyo
. Waandishi wetu katika jitihada za kumpata Wema ili kuzungumzia madai hayo, kwanza walifika nyumbani kwake tena ambapo safari hii walifunguliwa geti na mwanaume ambaye alisema staa huyo hayupo na kwa maelezo zaidi apigiwe simu. Wema alipopigiwa simu mara zote iliita bila kupokelewa. Jitihada za kumpata bado zinaendelea.