Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaasa wanaume wa wilaya ya Tarime kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuachana na kilimo cha bangi.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Serengeti, wilayani Tarime.
Waziri Mkuu amesema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kilimo cha bangi vinaitia doa wilaya hiyo, hivyo hawana budi wakaepukana navyo.
“Serikali inakemea vitendo vya ukatili, achaneni navyo. Mtu unamchapa mtoto makofi hadi anazimia, kitendo hicho hakiwezi kuvumilika na pia kinaitia doa wilaya yenu.”
Wakati Huohuo, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa wilaya hiyo, Glorious Luoga kuendelea na msako wa mashamba ya bangi na mirungi na kuchukua hatua kwa watakaobainika kuendesha kilimo hicho.
Amesema ardhi ya wilaya hiyo ni nzuri na inahimili kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kama mahindi, mihogo, ndizi, kahawa, pamba, ni marufuku kulima bangi.
Pia Waziri Mkuu ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wakandarasi waliotekeleza ujenzi wa maji mkoani Mara kwa sababu miradi hiyo wameijenga chini ya kiwango.
Waziri Mkuu amesema hayo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kupitia mabango wakidai kutonufaika na miradi ya maji katika maeneo yao licha ya Serikali kutoa fedha.
Wanaume Wanaopiga Watoto, Wanawake Waonywa na Waziri Mkuu
0
January 18, 2018
Tags