Wengi humfahamu kwa jina la Masoud Kipanya, lakini hilo si jina lake halisi, tunaweza kusema hilo ni jina lake la sanaa kwani limetokana na na katuni za Kipanya ambazo huwa anachora.
Jina lake ni i Ali Masoud, jina la Kipanya ni matokeo ya katuni ya Kipanya aliyoibuni zaidi ya miaka 28 iliyopita. Alizaliwa tareha 23 Juni 1972 jijini Dar es salaam.
Kipanya alianza kuchora katuni akiwa darasa la pili, na alianza kwa kuiga tu katuni za ndani na za nje kama ilivyo kawaida kwa yoyote anayeanza kufanya kitu, ila ‘professionally’ alianza rasmi mwaka 1988, huo ndio mwaka ambao katuni yake ya kwanza ilitoka katika gazeti la Heko.
Amewahi kufanya kazi kama mhariri wa katuni kwenye gazeti la Sanifu na mhariri mtendaji wa katuni gazeti la majira, pia katuni zake hutokea gazeti la Mwananchi.
Licha ya kujizolea umaarufu mkubwa katika uchoraji katuni, katika familia yake hakukuwa na mchoraji kabla yangu, isipokuwa baada ya yeye, mdogo wake naye ameshaanza kuja juu katika fani ya katuni. Licha ya kuwa wazazi wake si wachoraji, lakini mfumo wa maisha yao unatosha kabisa kusema nao pia ni wasanii.
Akizungumzia kazi yake ya uchoraji katuni, Kipanya alisema kuwa, changamoto kubwa anayokumbana nayo ni censorship. Kwa wasioelewa, censorship ni ile kitendo ambacho unachora katuni halafu kabla haijachapishwa inapitiwa na kama itaonekana ina madhara kwa mtu ama jamii Fulani, basi itarekebishwa ama isichapishwe kabisa.
Amesema hayo yamemtokea mara nyingi tu katika maisha yake akiwa katika magazeti mbalimbali. Mara nyingi censorship hutokea pale inapoonekana unachora katuni zinazosumbua mioyo ya walengwa hususani wanasiasa wasiopenda kukosolewa.
Alipoulizwa kama amewahi kupata misukosuko kutokana na katuni zake, Masoud alisema, “nakumbuka siku niliyomchora mtu mnene akiwa amemshika kamba iliyomfunga mbwa ambaye ameandikwa ‘polisi’, maana ya katuni hii ukiangalia kwa haraka haraka ni kwamba jeshi la polisi haliko kwa manufaa ya umma bali kwa manufaa ya watu wachache hasa viongozi wa chama tawala.Hiki kilikuwa ni kile kipindi ambacho wapinzani walikuwa wakibughudhiwa na polisi kila walipotaka kufanya mikutano yao ya hadhara.”
“La pili ni wakati ule mbunge mmoja aliyejulikana kwa jina la Tuntemeke Sanga alipokuwa anaumwa, nilichora katuni inayomuonyesha mheshimiwa Sanga akiwa amelazwa huku akiwa ametundikiwa damu, halafu pembeni yuko serikali akiwa amegeukia upande mwingine huku akivuta sigara kana kwamba hajali, bahati mbaya siku iliyofuata Mzee Sanga akafariki, naikumbuka siku hiyo vizuri, aliyekuwa katibu wa bunge wa wakati huo, Mzee Mlawa, alivamia ofisi za gazeti la majira, bahati nzuri, wakati anaingia mimi nikawa natoka, na pengine kutokana na umbo langu, hakuweza kudhani kwamba pengine huyu ndio masoud kipanya. Kilichoendelea kati yake na mhariri wangu kwa kweli sikukifahamu.”
“Alarm inaniamsha saa 11 alfajiri, naoga, navaa na kuelekea studio. Naanza kipindi saa 12 mpaka 3 asubuhi, baada ya hapo napumzisha akili kwa kama nusu saa kwa kupitia magazeti mbalimbali then naanza kufikiria wazo la katuni, wakati mwingine kama sina wazo hunichukua mpaka nusu saa kudevelop wazo la katuni, by saa 4 asubuhi naanza kuchora editorial cartoon. Huwa natumia mpaka masaa mawili kutegemeana na aina ya katuni, baada ya hapo, saa sita mchana namkabidhi dereva (wa taxi, sio wangu jamani) apaleke katuni ofisi za gazeti la mwananchi kwa ajili ya kesho yake. Baada ya hapo nageukia upande wa illustrations, mara nyingi huwa nina kazi za taasisi mbalimbali za ku-Simplify text into cartoons kwa ajili popular versions za machapisho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi. By saa 8 mchana huwa nimemaliza, kama kunakuwa na mikutano ofisini naingia, kwa kifupi by saa 10 jioni nakuwa nimemaliza ingawa wakati mwingine humaliza jioni zaidi, baada ya hapo narudi nyumbani kwa ajili ya kubadilisha nguo then naenda mazoezini. Nikitoka mazoezini huwa sitoki tena nyumbani,” alisimulia Kipanya wakati akijibu kuhusu ratiba yake kwa siku.
Kipanya, ameshiriki maonyesho mbalimbali Tanzania na Afrika Kusini kama mtaalam wa matumizi ya rangi ‘Painter’ na amejishindia tuzo nyingi ikiwa pamoja na tuzo ya kwanza ya katuni Afrika Mashariki.
Mbali na kuchora katuni, Kipanya ni mtangazaji wa kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, ni mwanamitindo lakini pia ndiye mbunifu wa vipindi vya runinga vya ‘Maisha Plus’ na ‘Inawezekana.’