Jumla ya Watu 456, wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 700 wamejeruhiwa mkoani Mbeya kutokana na matukio ya ajali za barabarani katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2017.
Akizungumza hali ya usalama ya mkoa kwa mwaka 2017 mbele ya waandishi wa habari Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga amebainisha kuwa jumla ya makosa 82,211 ya ukiukwaji wa sheria za barabarani yalipatikana katika kipindi cha mwaka 2017, wakati mwaka 2016 yalikuwa ni 66,172.
Kamanda Mpinga, alisema Mwaka jana jumla ya watu 170 walipoteza maisha kutokana na ajali za barababani wakati mwaka 2016, watu waliopoteza maisha ni 286 hivyo kuna upungufu wa asilimia 40.5 ya idadi ya vifo vilivyolipotiwa katika kipindi cha miaka miwili.
“Sababu za kutokea kwa matukio ya ajali ni kuongezeka kwa vyombo vya usafiri mkoani Mbeya hasa magari na pikipiki, baadhi ya madereva kutozingatia sheria za usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na mwendokasi hasa usiku na ulevi licha ya jitihada za jeshi la polisi kwa kushirikiana na wadau kutoa elimu mara kwa mara” alisema.
Akizungumzia hali ya uhalifu, kamanda Mpinga alisema jumla ya makosa 26,009 yaliripotiwa kutokea katika mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha mwaka jana ikilinganishwa na matukio 32,943 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2016.
Aidha Kamanda Mpinga amesema kwa mwaka 2018 jeshi la polisi limeandaa mikakati mbalimbali ya kukabiliana na wahalifu na uhalifu pamoja na kupunguza ajali za barabarani ikiwa ni pamoja na kubaini muelekeo wa uhalifu na maeneo tete ili kuelekeza nguvu katika maeneo hayo.