Watu Wengi Wajitokeza Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Kupata Msaada wa Kisheria

Watu Wengi Wajitokeza Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Kupata Msaada wa Kisheria
Wananchi hao wametoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, huku baadhi wakitoka Rufiji mkoani Pwani ambao wameandaliwa utaratibu maalumu.

Baadhi yao wamesema leo Jumatatu Januari 29,2018 kuwa migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na wenyeviti wa mitaa wanaopokea rushwa na kuwapendelea wenye fedha nyingi.

Mkazi wa eneo la Chasimba wilayani Kinondoni, Bakari Mussa amesema mgogoro kati yake na aliyevamia kiwanja chake uliamuliwa na Mahakama naye alishinda lakini amejitokeza mtu wa tatu anayedai aliuziwa eneo hilo na aliyeshindwa kesi.

"Tumekuja kupata msaada wa kisheria kuhusu masuala ya ardhi, tumeshindwa kuendeleza ardhi yetu kwa sababu ya zuio la Mahakama aliloweka huyo mtu. Ninatarajia kupata msaada kutoka kwa mkuu wa mkoa," amesema Mussa.

Kiongozi wa timu ya wanasheria, Georgia Kamina amesema mwamko wa wananchi ni mkubwa na waliojitokeza wote watasikilizwa.

Amesema timu yake ina wanasheria 150 kutoka Shule ya Sheria, ustawi wa jamii, maofisa kazi, Jeshi la Polisi na wanasheria wengine wa kujitegemea, hivyo wana uwezo wa kuwamudu wote.

Kamina amesema wengi waliosikilizwa wana matatizo ya ardhi, mirathi na ajira, ambao baada ya kusikilizwa hupewa ushauri wa kitaalamu wa namna ya kumaliza matatizo yanayowakabili.

"Tutatoa huduma wiki nzima kuanzia leo Januari 29 hadi Februari 2,2018. Tumejitolea kumsaidia mkuu wa mkoa kuifanya kazi hii," amesema.

Awali, akizungumza na wanasheria hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka kutohukumu wananchi wanaowasikiliza badala yake watoe ushauri wa kitaalamu.

Amesema mwisho wa siku waandae ripoti kumshauri hatua za kuchukua zilizo ndani ya mamlaka yake na kubainisha njia nyingine zilizo nje ya mamlaka yake.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad