Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambao umedumu kwa miaka miwili.
Ametoa uamuzi huo jana jioni, wakati akizungumza na watumishina madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja na Halmashauri ya Mji wa Mbinga kwenye ukumbi wa jumba la Maendeleo mjini Mbinga.
“Ninazo taarifa kuwa kuwa mnagombea mahali pa kujenga makao makuu ya Halmashauri hali mnataka kujenga kwenye chanzo cha maji. Hiyo haikubaliki. Kwenye vyanzo vya maji hakujengwi miji tena Afisa Maliasili nenda ukapande miti zaidi ili tutunze chanzo chetu,”alisema Waziri Mkuu.
Wataalamu wa Halmashauri hiyo walikuwa wakivutana na Madiwani juu ya makao makuu hayo kujengwa ,Ndengu ambako ni karibu na chanzo cha maji huku wengine wakitaka yajengwe Kigonsera kwa madai kuwa kote ni karibu na wananchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga iligawanywa Julai 215 kwa kupata Halmashauri ya Mjiwa Mbinga na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na ilianza kazi Julai 2016.
Waziri Mkuu alisema Halmashauri hiyo si ya kwanza kuwa na migogoro kwa hiyo nimeamua mjenge hapa hapa mjini Mbinga. Mkijenga huko wanakotaka hawa mtagombana na mkijenga kule nako pia mtagombana lakini ugomvi wenu ni kwaajili ya nani? Kama sikuwaumiza wananchi mnaowaongoza ni nini?,alihoji Waziri Mkuu.
“Miaka yote mmekuwa mkipata huduma kutokea hapa hapa kabla Halmashauri hizi hazijatenganishwa. Tumeleta fedha mara mbili mara ya kwanza sh. milioni 500 na ya pili sh. milioni 400 lakini hazijatumika kwasababu ya migogoro yenu isiyo na tija. Kwa hiyo makau makuu yatajengwa hapa hapa mjini,” alisisitiza Waziri Mkuu.