Waziri Mkuu: “Tutakamilisha ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Musoma”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inakamilisha ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyoanza kujengwa mwaka 1980.

Alitoa kauli hiyo wakati alipokagua ujenzi wa hospitali hiyo baada ya kuwasili mkoani Mara kwa ajili ya ziara yake ya kikazi.

Waziri Mkuu amesema Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa awamu, ambapo wataanza na eneo la mapokezi na vyumba vya madaktari.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya nchini, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.

Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imetoa sh. bilioni 1.4 ili ujenzi uendelee. Ujenzi huo ulianza mwaka 1980, ulisimama mwaka 1987 kuanza tena 2010.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekagua uwanja wa ndege wa Musoma mkoani Mara ambao unatarajiwa kukarabatiwa na kuwekwa lami.

Amesema kukamilika kwa ukarabati huo wa kiwanja hicho kutafungua fursa za utalii ndani ya mkoa huo ambao umezungukwa na vivutio vingi.

Amesema Serikali imedhamilria kukarabati viwanja mbalimbali vya ndege nchini kikiwemo cha Musoma ili kuboresha huduma za usafiri wa anga.

Viwanja vingine vinavyotarajiwa kukarabatiwa ni Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Lindi, Moshi, Njombe, Tanga, Simiyu, Singida na Songea.

Waziri Mkuu amesema viwanja hivyo kwa sasa vinakarabatiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ambao wanajenga kwa gharama nafuu na kwa viwango vinavyostahili.

Awali, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Mara Mhandisi Mlima Ngaila alisema ukarabati huo utafanyika kwa awamu tatu ambapo ya kwanza itahusisha upanuzi wa uwanja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege.

Alisema barabara ya kuruka na kutua ndege ina urefu wa km. 1.6 na upana wa mita 33 ni ya changarawe, hivyo kusababisha baadhi ya ndege kushindwa kutua.

Pia, Waziri Mkuu alikagua ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma na kwamba ameridhishwa na ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo.

“Shule hii ilipewa sh bilioni 1.28 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu. Nimekagua jengo la utawala, madarasa, mabweni, jiko, maabara na bwalo, nimeridhika na kazi iliyofanyika.”

Shule hiyo ni miongoni mwa shule 10 kongwe ambazo Serikali iliamua kuzikarabati ili ziweze kurudi kama zamani na kuendelea kutumika.

Hata hivyo Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Musoma kushirikiana na uongozi wa shule hiyo katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili.

Miongoni mwa changamoto hizo ni malipo ya watumishi wasaidizi wakiwemo wapishi, walinzi na madereva, ambapo aliitaka kuchukua jukumu la kuwalipa watumishi hao badala ya kuacha jukumu hilo kwa Mkuu wa Shule.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad