Hakimu Michael Mteite aliyemhukumu kifungo cha miezi mitano jela mbunge
wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ameanza likizo jana.
Mteite, ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mbeya, alitoa hukumu hiyo juzi kwa Sugu pamoja na katibu wa Chadema
Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga baada ya kuwatia hatiani kwa kutumia
lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Sugu na Masonga walitoa kauli hiyo Desemba 30 mwaka jana katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini
Mbeya.
Hakimu huyo alipopigiwa simu jana na mwandishi wa Mwananchi aliyetaka
kujua kuhusu uwepo wake likizo, kabla hata ya kuelezwa hilo alimtaka
kuwasiliana na Msajili wa Mahakama.
Hata alipotumiwa ujumbe wa maneno (sms) kujulishwa kwamba msajili
alishalizungumzia hilo na kilichohitajika ni kauli yake, hakujibu.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, naibu msajili
mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, George Herbert alisema Hakimu
Mteite amechukua likizo kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa utumishi
kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma pindi muda wao unapokuwa
umefika.
“Ni likizo yake ya mwaka… na amechukua likizo kama mtumishi mwingine
ambaye anaweza kuchukua likizo muda wake unapokuwa umefika. Kimsingi ni
kwamba amechukua likizo ya muda wa wiki tatu kuanzia leo (jana) na ni
likizo huwa anachukua kila mwaka muda unapokuwa umefika.
“Hivyo suala la kusema kwamba eti amechukua likizo kwa sababu ya hukumu
aliyoitoa jana (juzi) haina msingi wowote, bali ni haki yake kuchukua
likizo hiyo. Inapofika Februari kila mwaka huchukua likizo yake na huwa
inategemea majukumu anayokuwa amepangiwa kuyafanya,” alisema naibu
msajili.
Taarifa ya kusudio la rufaa
Akizungumzia taarifa ya kusudio la mawakili wa Sugu na Masonga kukata
rufaa dhidi ya hukumu hiyo na kuomba dhamana kwa wateja wao, Naibu
Msajili Mfawidhi, Herbert alisema baada ya hukumu kutolewa juzi,
mawakili hao walianza mchakato wa kukata rufaa na siku hiyohiyo
walipatiwa nakala ya hukumu.
Alisema kilichokuwa kikisubiriwa hadi jana ni nakala za mwenendo wa kesi ili kukamilisha utaratibu wa kukata rufaa.
Herbert alisema kukata rufaa ni haki ya mlalamikaji anapoona hajaridhishwa na hukumu.
Alisema, “Kinachofanyika ni kuhakikisha wanapatiwa mwenendo wa shauri na
hilo lipo hatua za mwisho kukamilika kwa sababu wameshapata nakala ya
uamuzi ulitolewa jana ileile,” alisema.
Mke wa Sugu, Masonga walonga
Happy Msonga ambaye ni mke wa Sugu na Grace Mallya wa Masonga
wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema wanajua fika hukumu ilitolewa
kwa mrengo wa kisiasa, hivyo hawakubaliani na adhabu waliyopewa waume
wao.
Grace alisema, “Ukiachilia mbali ndani ya familia tu, lakini wale watu
wa nje wanavyo ‘comment’ unaona kabisa hakuna haki iliyotendeka.”
Alisema anazidi kumuombea mume wake aendelee kuwa na nguvu na imara
zaidi katika kipindi chote anachopitia kwa kuwa ana imani hayo ni mapito
na yatakuwa na mwisho ambao huwa ni ukombozi katika harakati za
kisiasa.
Happy alisema walitarajia kilichotokea kwa kuwa walishaona dalili
mwanzoni baada ya hakimu kukataa kujitoa wakati washtakiwa
walishamkataa.
Alisema wana imani na mawakili, Peter Kibatala na Faraji Mangula kwamba
watafanikiwa kukata rufaa kwa ajili ya uamuzi mwingine. Alisema kwa sasa
wanawaombea kwa Mungu, Sugu na Masonga waendelee kuwa na afya njema.
Wakati Sugu akitumikia adhabu ya kifungo, mama yake mzazi Desderia Mbilinyi imeelezwa na familia kuwa ni mgonjwa.
Wasemavyo wapigakura Mbeya
Akizungumzia hukumu iliyotolewa kwa Sugu na Masonga mkazi wa Uyole,
Bahati Longopa alisema Mahakama imetenda haki kulingana na vifungu vya
sheria. Hata hivyo, alisema ni vyema ingetoa hukumu ya kifungo cha nje
ili mbunge huyo aweze kuwatumikia wananchi katika shughuli za maendeleo.
Mkazi wa Sabasaba, John Mbika alisema ni mapema kuzungumzia hilo hivyo ni vyema Mahakama ikaachiwa iendelee na kazi.
Mkazi wa Nonde, Rehema Mwanjonde alisema Mahakama imetenda haki kwa
mujibu wa sheria lakini akaitaka Chadema ikate rufaa ili Sugu aweze
kuwatumikia wananchi na kusimamia shughuli za maendeleo.
Hoja sita za Lissu
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akizungumzia hukumu hiyo katika waraka alioutoa juzi aliibua hoja sita.
Lissu anayeendelea na matibabu nchini Ubelgiji katika hoja ya kwanza
alisema hukumu hiyo si mwisho wa mjadala mahakamani na kwamba bado kuna
fursa na haki ya rufaa Mahakama Kuu na ikibidi Mahakama ya Rufaa.
Pili, alisema hukumu hiyo haina maana Sugu atakaa gerezani muda wote,
kwamba kuna haki ya dhamana (pending appeal) na kubainisha kuwa hivyo
ndivyo walivyofanya kwa viongozi na wanachama wengi wa Chadema.
Katika hoja ya tatu, Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema
alisema hukumu ya Sugu haina athari yoyote kwa mbunge huyo kuhusu
kugombea tena au kupoteza ubunge wake kwa sababu Katiba inaweka masharti
ya kifungo cha miezi sita au zaidi na kwa makosa ya utovu wa uaminifu.
“Uchochezi au kutoa lugha ya matusi sio makosa ya utovu wa uaminifu,” alisema.
“Nne, pamoja na kwamba sijaona nakala ya hukumu, adhabu ya kifungo bila
faini kwa kosa la kwanza ni kinyume na ‘sentencing principles’. Hii ni
mojawapo ya hoja zetu zilizoshinda katika kesi ya Peter Lijualikali
(mbunge wa Kilombero) Mahakama Kuu mwaka jana,” alisema.
Tano, Lissu alisema hata kama Sugu atakaa gerezani muda wote huo (wa
miezi mitano), hukumu za kesi za kisiasa kama hiyo hazijawahi
kuwapunguzia heshima wapigania haki popote duniani.
Jambo la sita alisema, “Naunga mkono pendekezo la Zitto (Kabwe-mbunge wa
Kigoma Mjini) kwamba wabunge wetu wote warekodi maneno aliyofungiwa
nayo Sugu na kuyaweka mitandaoni ili watukamate na sisi pia, mpaka
wakimbie wenyewe au watukamate na kutufunga wote.”
Mkishinda Haki imetendeka , mkishindwa haki haijatendeka, hivyo haki kwenu ni kushinda tu.
ReplyDelete