Ligi kuu soka Tanzania Bara inaendelea leo kwa mchezo mmoja ambapo Azam FC watakuwa ugenini mkoani Iringa kucheza na wenyeji wao Lipuli FC kwenye uwanja wa Samora mjini humo.
Azam FC leo watakuwa wanasaka ushindi wa kwanza ndani ya mechi tatu, baada ya Februari 7 kufungwa 1-0 na Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 1-1 na wenyeji, Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kwa upande wao Lipuli FC inayofundishwa na nyota wa zamani wa Simba SC, Amri Said na Suleiman Matola, wametoka kushinda mechi moja kati ya 10 zilizopita, wakifungwa tano na sare nne hivyo nao watakuwa wanataka kuutumia uwanja wa nyumbani vizuri.
Kikosi cha Azam FC kimepata nguvu mpya kuelekea mchezo wake wa leo baada ya wachezaji wake wawili waliokosa mechi mbili zilizopita, Nahodha msaidizi Aggrey Moris, aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano na mshambuliaji Yahya Zayd wote kurejea kikosini.
Mchezo huo ni wa raundi ya 19 ambapo Azam FC inashika nafasi ya tatu kwa pointi 34 nyuma ya Yanga yenye alama 37 katika nafasi ya pili na vinara Simba wakiwa kileleni kwa pointi 42. Lipuli FC inashika nafasi ya 9 na alama 19.