Matarajio ya filamu ya ‘Black Panther’ kufanya vizuri yameanza kuonekana katika siku tatu tangu ilipoachiwa Ijumaa iliyopita mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Filamu hiyo imetajwa kuingiza kiasi cha dola milioni 192 ambapo kwa fedha za kitanzania ni zaidi ya shilingi bilioni 432 kwa nchini Marekani.
Kutokana na kiasi hicho kilichoingiza filamu hiyo, kimevunja rekodi zilizowahi kuwekwa na filamu kibao kwenye box office, ikiwemo ile iliyowahi kuwekwa April mwaka jana na The Fate of the Furious, iliyoongozwa na Felix Gary Gray.
Wakati huo huo kampuni ya The Walt Disney Company yenye makao yake makuu mjini California, Marekani, inakadiria kuwa Black Panther itaingiza kiasi cha Bilioni 491 za kitanzania ndani ya siku nne kwa Marekani pekee.
Filamu hiyo pia imeingiza kiasi cha Bilioni 813 za Kitanzania kutoka sehemu zingine duniani. Pia Black Panther imekuwa filamu ya pili kutoka kwenye kampuni ya Marvel kuwa na ufunguzi mkubwa zaidi ikiongozwa na filamu ya The Avengers ya mwaka 2012.
Black Panther imewakutanisha waigizaji kama Chadwick Boseman ambaye ndio staa wa filamu hiyo, Lupita Nyong’o ambaye asili yake ni mkenya japo alizaliwa Mexico na kukua nchini Kenya, Michael B. Jordan, Danai Gurira, John Kani na Connie Chiume.