Pia, chama hicho tawala kimelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linalinda amani wakati wote wa uchaguzi huo ili wananchi wakawachague viongozi wanaowapenda na wasiruhusu hila zozote.
Hayo yamesemwa leo Februari 15,2018 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, lepHumphrey Poole alipozungumza na waandishi wa habari ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam.
"CCM inawachama wasiopungua milioni 12. Tanzania ina wananchi wasiopungua milioni 50 na wapiga kura wa Taifa zima ni milioni 25. Tunapokwenda katika uchaguzi, wenzetu wanapaswa kulitambua hili," amesema Polepole,
"Ushindi ni sayansi, ukiondoa wanachama wetu na kazi ya siasa ambayo tunaifanya, tumefanya kampeni jimbo zima, kata nzima, mtaa wote, kaya, kitanda kwa kitanda na mtu kwa mtu. Baada ya haya tunakamilisha kuandaa sherehe ya kusheherekea ushindi."
Kwa msisitizo, Polepole amesema: "Kwa namba hii CCM itakuwa na ushindi mkubwa na wa kishindo na hii tutakuwa tunatesti mitambo kwa uchaguzi mkuu 2020 na ule wa serikali za mitaa."
Amewasihi vyama vya upinzani kuwa tayari kushindwa akisema, “kwa hiyo wawe tayari kushindwa kwani wamezoea kushindwa na kwa hesabu hizo hapo juu tushashinda."
Kuhusu wagombea katika uchaguzi huo, Polepole amesema: "Wagombea hawa 12, wawili wa majimbo na 10 wa Kata. Kinondoni - Maulid Mtulia na Dk Godwin Mollel kule Siha na madiwani ni makini kwelikweli ambao watashughulika na matatizo ya wananchi na hawa ndio wataibuka washindi."
"Uteuzi wa wagombea hawa haukufanyika kiholela, unazingatia Katiba na kanuni za Chama. Wagombea wote wamepitishwa katika matanuru ya kupimwa kwa hatua mbalimbali na hakika ni watu waadilifu, wachapa kazi."
Polepole amesema kuna taarifa wamezipata kwamba kuna mkakati unaandaliwa na wapinzani wa kutoa watu mikoani ili waje kuharibu uchaguzi huo ambao hawatakubali hilo litokee.
"Tumelijulisha Jeshi la Polisi juu ya nyumba hizo na watu hao. Sisi tumefanya yetu tumemaliza. Kura hazilindwi na watu, kwa mujibu wa taratibu za kisheria uko utaratibu," amesema Polepole na kuongeza:
"Uchaguzi ni sehemu ya wananchi kuchagua. Vyombo vyenye mamlaka ya kuhakikisha amani inakuwapo na wananchi wawachague viongozi wanaowapenda. Hatuliagizi Jeshi la Polisi, lakini sisi ndio chama kinachoongoza nchi."