Wakuu wa mikoa Arusha na Manyara wamewataka walimu wa shule za msingi na sekondari katika mikoa hiyo kutopokea michango yoyote kutoka kwa wazazi, watakaobainika watachukuliwa hatua kali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Februari 1, 2018 Mrisho Gambo wa Arusha na Alexander Mnyeti wa Manyara wamesema kukusanya michango hiyo ni kwenda kinyume na mpango wa elimu bure.
Gambo ametoa kauli hiyo katika kikao na wadau wa elimu wilaya ya Karatu, kubainisha kuwa imeibuka tabia ya baadhi ya wakuu wa shule kushirikiana na bodi za shule kubuni utitiri wa michango.
Mwenzake Mnyeti akiwa katika ziara ya siku saba wilayani Simanjiro, amepiga marufuku michango hiyo na kuacha maagizo kwa wananchi, walimu na viongozi wa ngazi ya wilaya na vitongoji.
Mnyeti amemtaka mkuu wa shule ya sekondari Orkesumet, Ighnas John ahamishwe kwa madai kuwa mmoja wa wazazi amemlalamikia kuwa anachangisha fedha za kuwalipa walimu wa ziada wa Sayansi wakati shule hiyo ina walimu wa kutosha.
Akiwa katika mkutano wa hadhara kwenye mji mdogo wa Mirerani, Mnyeti aliwaita jukwaani wakuu wa shule za sekondari Mirerani Benjamini Mkapa na Naisinyai na walimu wakuu wa shule za msingi Mirerani, Songambele, Jitegemee, Tanzanite na Endiamtu na kuwaonya juu ya michango hiyo.
"Kazi ya mwalimu ni kufundisha, hata mimi nimeshawahi kuwa mkuu wa shule, natambua namna wengine wanavyoongeza idadi ya wanafunzi ili fedha za ruzuku za shule zinazotolewa zipelekwe nyingi katika shule zao,” amesema.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Jitegemee, Leah Eliminate amesema hawachangishi michango na kubainisha kuwa inayochangwa ni kwa ajili ya chakula cha wanafunzi, hukusanywa chini ya usimamizi wa kamati ya shule.
Naye mkuu wa shule ya sekondari Mirerani Benjamini Mkapa, Emmanuel Kallo amesema bodi ya shule iliunda kamati inayosimamia suala la chakula kwamba, huku akikanusha shule hiyo kuchangisha fedha.
Hata hivyo, Mnyeti alipinga jambo hilo na kubainisha kuwa kuchangia chakula ni hiari ya mzazi.
Amesema ni marufuku walimu kuchangisha fedha na kama kamati za shule na bodi zikiona kuna ulazima zitoe michango ofisi za kata